Waangalizi wa ndani wazipe uzito chaguzi ndogo nchini

Muktasari:

  • Wakati wa uchaguzi uliotangulia wananchi walishiriki katika hatua tofauti kuanzia elimu kwa mpiga kura, mikutano ya kampeni na hata kukutana na waangalizi wa uchaguzi waliowapa uhuru wa kutoa maoni yao wakielezea mwanga au giza mbele yao.

Kuna tofauti kubwa ukirejea wananchi wa Kata ya Buhangaza wilayani Muleba waliposhiriki kupiga kura za Uchaguzi Mkuu mwaka 2015 na pale waliposhiriki uchaguzi mdogo Februari 17, 2018 baada ya aliyekuwa diwani wao, Samsoni Makoti kufariki dunia.

Wakati wa uchaguzi uliotangulia wananchi walishiriki katika hatua tofauti kuanzia elimu kwa mpiga kura, mikutano ya kampeni na hata kukutana na waangalizi wa uchaguzi waliowapa uhuru wa kutoa maoni yao wakielezea mwanga au giza mbele yao.

Katika kata ileile wakati wa uchaguzi mdogo hakuna mwangalizi wa uchaguzi aliyeonekana kufuatilia hatua kwa hatua matukio yote ambayo taarifa zake ni msaada kwa Tume ya Taifa ya Uchaguzi na wadau wengine kwa ajili ya kuboresha chaguzi zinazofuata.

Buhangaza ni miongoni mwa kata chache nchini ambazo mgombea aliyeongoza kwa kura katika vituo saba kati ya tisa anaweza kuukosa ushindi. Haya ni maajabu yaliyotakiwa kushuhudiwa na waangalizi wa uchaguzi na kumbukumbu zake kuwekwa kwenye taarifa kwa ajili ya rejea.

Waangalizi wa ndani wanaonekana kuzipa kisogo chaguzi ndogo za madiwani na wabunge katika maeneo mbalimbali nchini, ikilinganishwa na wingi wao wakati wa Uchaguzi Mkuu.

Kukosekana kwa kundi hili wakati wa chaguzi zinazoendelea ni kushindwa kujua changamoto zinazojitokeza, hivyo wadau hawawezi kuwa na hoja thabiti za kuwashauri waandaaji wa uchaguzi kwa kuwa hakuna ushahidi kutoka kwenye maeneo ya kupigia kura.

Chaguzi hizi zinatakiwa kupewa uzito uleule kwa kuwa zina tafsiri kubwa kwenye maisha ya wananchi ambao huwapoteza wawakilishi wao kwa sababu mbalimbali, mfano vifo na wengine kujivua uanachama na kujiunga na vyama vingine.

Mwananchi aliyemchagua diwani wake katika Uchaguzi Mkuu uliopita na kushangilia matokeo kwa furaha, baada ya miaka miwili anamuona diwani yuleyule akijivua uanachama wa chama cha awali na kutaka achaguliwe tena kupitia chama kingine, anahitaji kusaidiwa.

Majukumu ya waangalizi wa uchaguzi hayatakiwi kuishia kwenye chaguzi za rais, wabunge na madiwani zinazofanyika kwa wakati mmoja ambapo huonekana kwa wingi wakiwa wamegawana majukumu kuanzia mijini hadi vijijini.

Waangalizi wa uchaguzi ndio wanatakiwa kueleza kwa kina na ushahidi jinsi mpiga kura anavyoweza kufanya uamuzi wa kumchagua kiongozi anayemtaka kwa uhuru huku vituo vya kupigia kura vikiwa vimezungukwa na askari waliojihami kwa virungu na mitutu ya bunduki.

Baada ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015, mwavuli wa waangalizi wa ndani (Cemot) kupitia kwa Mwenyekiti mwenza, Martina Kabisama ulitoa tathimini yake baada ya kupokea taarifa kutoka maeneo yote nchi walipopeleka waangalizi.

Wingi wa askari ambao kwa vyovyote vile hujenga hofu kwa wapiga kura, matumizi ya rasilimali za umma wakati wa kampeni na ucheleweshaji wa vibali kwa waangalizi kutoka Tume ya Uchaguzi ni miongoni mwa changamoto zilizobainishwa.

Kwa kuwa Tume ya Taifa ya Uchaguzi tayari imetangaza uchaguzi katika kata 77 nchini na Jimbo la Buyungu mkoani Kigoma utakaofanyika Agosti 12, 2018, pia waangalizi wa ndani kupitia mwavuli wao wanatakiwa kushiriki katika hatua zote kama chachu ya kuongeza uwazi katika uwanja wa demokrasia.

Phinias Bashaya ni Mwandishi wa Mwananchi Bukoba.