Monday, June 11, 2018

Wachezaji, makocha Kombe la Dunia ni darasa toshaIbrahim Bakari

Ibrahim Bakari 

Fainali za Kombe la Dunia zinaanza Alhamisi wiki hii kwa timu mbili kukata utepe.

Mpambano wa kwanza, wenyeji Russia watacheza na Saudi Arabia.

Inasemwa kuwa ni timu dhaifu kwa kuwa imepoteza mechi zake nyingi za majaribio, ikiwemo waliyofungwa mabao 2-1 na Ujerumani.

Hata kocha wa Ujerumani, ametilia wasiwasi timu yake, wakati Saudi Arabia inaonekana kuwa timu dhaifu, Joachim Low anasema wasiwasi wake ni kama timu yake itatetea ubingwa.

Iliifunga kwa mbinde Saudi Arabia mechi za kupasha kabla ya kuanza kwa michakato ya Kombe la Dunia.

Zipo timu nyingi ambazo zitaaga mapema, zipo ambazo zitaishia katikati na zile zitakazoingia fainali.

Kuna zitakazofanya maajabu, timu haikupewa nafasi lakini ikapenya na kufika mbali.

Si ajabu fainali za mwaka huu zikashuhudia timu vipenzi zikiaga mapema kabisa na hata kuondosha ladha ya mashindano, lakini soka ndivyo ilivyo. Lazima baadhi ya timu zitoke ili wengine wasonge mbele.

Mpira una hali tatu, kufungwa, kushinda na kutoka sare.

Kuanza kwa fainali hizo kuna mengi, wapo watakaokuwa wakivuna pesa kwa kuonyesha mpira na mengine mengi.

Lakini mimi ninadhani ni wakati wa makocha na wachezaji makini kutuliza akili na kuchukua mechi za Kombe la Dunia kama darasa.

Mwezi mmoja wa kushuhudia fainali hizo ni wa kutosha kwani kuna mechi zaidi ya 60 za kujifunza.

Kwa makocha kuna kujifunzo mifumo mbalimbali ya timu, kuona upi una faida na upi ambao kama ukitumika pia unaweza kuleta faida.

Makocha si kwenda au si kukaa na kushabikia timu. Hapa ni kuchukua mbinu na kuona aina ya soka linalopigwa na timu moja na nyingine katika fainali hizo.

Kwa mbinu, njia zote hizo zinatengeneza mfumo ambao kama wakitumia kwa wachezaji wao, iwe kwa timu kubwa ama ndogo, italeta mafanikio, labda kocha asijue jinsi ya kuusoma mchezo.

Kingine ninachokiona ni kwa wachezaji wenyewe.

Bila kuweka ushabiki, kuanzia makipa, mabeki, viungo na washambuliaji, kuna mengi ya kujifunza.

Wakati gani sahihi wa kufanya uamuzi, wakati gani sahihi wa kuacha kufanya uamuzi, nini kifanyike kwa wakati gani.

Makipa wasome mbinu na jinsi ya kulinda milango, wakidaka wanafanya nini baada ya hapo.

Kwa mabeki, ni wakati gani kuna presha na wakati gani hakuna na nini cha kufanya kwa wakati gani.

Kwenye viungo. Kuna mengi ambayo ni ya darasa kwa jumla.

Kwa mifumo mbalimbali ya soka, siku hizi viungo wanafanya kazi gani, wanakwendaje, vyote hivyo ni wachezaji wenyewe kujifunza kutokana na wachezaji wa timu mbalimbali.

Inapendeza kusoma kwa kuwa michezo inafuatana tofauti na zile mechi za kila baada ya muda.

Kwa washambuliaji. Tatizo la kufunga, linamalizwa vipi, wakati gani mchezaji anapiga golini, wakati gani wa kuua offside.

Je, mipira iliyokufa karibu na goli inapigwaje hadi kufunga, penalti zinatengenezwaje bila kujitupa na kupata kadi.

Vyote hivyo tunavitaraji kubadilisha wachezaji, lakini kwa wenye dhamira ya dhati kutaka kujifunza. Kombe la Dunia litumike kama darasa na matokeo tuyaone.

-->