Wagundua programu mpya ya simu itakayowasaidia watu wenye VVU

Muktasari:

  • Bara la Afrika ndilo linaloandamwa zaidi na ongezeko la maambukizi mapya ya virusi vya Ukimwi huku wanasayansi wakionya kuwapo uwezekano wa hali kuwa mbaya zaidi iwapo kutakosekana utashi wa kiasi wa kukabiliana na janga hilo.

Wanasayansi barani Afrika wameanza kuchukua hatua ambazo kukamilika kwake zinaweza kuwapunguzia usumbufu watu walioathirika na virusi vya Ukimwi na tayari wanatumia dawa za kukabiliana na makali ya virusi hivyo.

Bara la Afrika ndilo linaloandamwa zaidi na ongezeko la maambukizi mapya ya virusi vya Ukimwi huku wanasayansi wakionya kuwapo uwezekano wa hali kuwa mbaya zaidi iwapo kutakosekana utashi wa kiasi wa kukabiliana na janga hilo.

Kutokana na ukubwa wa tatizo, zaidi ya wanasayansi 16 kutoka Bara la Afrika wameshiriki katika shindano la kutafuta ufumbuzi kwa changamoto zinazoonekana kuwa kubwa zaidi zinazoikumba jamii barani Afrika.

Wakiwa na shauku ya kuchangia majibu katika kutatua changamoto hizo, wanasayansi hao hivi karibuni walikutana Kigali, nchini Rwanda kukamilisha shindano maalumu la kuunda programu ya simu kwa ajili ya wagonjwa wa ukimwi. Utafiti wao kupitia shindano umefanyika kwa kipindi cha miaka mitatu sasa.

Miongoni mwa viongozi wa wataalamu hao, Joel Gasana ambaye ni mwanafunzi wa matibabu katika Chuo Kikuu cha Mjini Kigali, anasema programu hiyo ya simu itawasaidia waathirika wa ukimwi kufuatilia matibabu yao.

Mwana teknolojia huyo ambaye ameunda programu hiyo (app), anasema wengi waliokuwapo kwenye timu hiyo wana matumaini makubwa ya kufanikisha ajenda yao na hivyo kuwasaidia kutua mzigo wale wanaugua ugonjwa huo.

“Kwa mfano nchini Rwanda, viwango vya maambukizi ya ukimwi vipo juu sana... ukiangalia takwimu zinaonyesha asilimia 3.3 ya idadi ya watu wameambukizwa,” anasema.

Utafiti uliopo unaonyesha asilimia 27 ya watu walioambukizwa hawazingatii matibabu yanayohitajika jambo linalowafanya watumbukie katika janga zaidi.

Hali hiyo ndiyo iliyowasukuma wataalamu hao kuunda programu hiyo ili kuhakikisha wagonjwa wote wanazingatia matibabu

Gasana anasema: “Kusanyiko letu mjini Kigali limeniinua kutoa mchango mkubwa katika tatizo hili. Programu yangu imekubaliwa na Wizara ya Afya na kituo cha biolojia cha Rwanda. Tutakutana na maofisa wiki ijayo ili kuanzisha ushirikiano,” anafafanua.

Timu hiyo imechaguliwa kushiriki katika mashindano ya tuzo ya uvumbuzi wa jukwaa la Einstein, itakayofanyika baadaye mwaka huu nchini Rwanda.

“Jukwaa lijalo la Einstein, linatajwa kuwa kubwa zaidi na litawaleta pamoja wanasayansi kadhaa kutoka barani Afrika watakaojadili uvumbuzi na jinsi ya kutatua changamoto zinazolikumba Bara la Afrika,” anasema.

Wakati akifungua sherehe iliyowakutanisha wataalamu hao 16, Rais Paul Kagame wa Rwanda alisema, “Kwa muda mrefu, Bara la Afrika limekubali kuachwa nyuma lakini hali hii imeanza kubadilika jinsi tunavyoona katika jukwaa hili.”

Naye mtaalamu wa masuala ya teknolojia na nishati safi, Dk Rose Mutiso anasema mwamko unaonyeshwa na wataalamu hao na jinsi wanavyofanya kazi kwa ushirikiano, kuna kila matumaini ya mkakati huo kuzaa matunda yanayosubiriwa.

“Nadhani ni jambo la kufurahisha na kuchochea kuona kwamba jamii hii ipo, inakua pamoja na kwa mshikamano tulionao tunajiona tupo sehemu ya jamii ya wanasayansi wa kimataifa,” anasema.

Baadhi ya wataalamu hao wameanza kuzifanyia majaribio baadhi ya kazi walizozifumbua na sehemu ya ishara ya uwezekano wa kupatikana mafanikio. “Nakaribia kumaliza uvumbuzi wangu. Naomba mnitakie kila la kheri,” anasema.

Ingawa mradi huo umelenga kuwaletea ufumbuzi wale wanaokabiliwa na changamoto za kutozingatia matibabu ya virusi vya HIV, wagunduzi wengine kwenye kusanyiko hilo wamekwenda mbali zaidi wakibuni njia za kukabiliana na matatizo mengine kama ya saratani.

Wataalamu hao wanakuna vichwa kunoa bongo zao huku ripoti za kimataifa zikisema nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahara ndiyo zimekuwa zikiathiriwa zaidi na virusi vya Ukimwi.

Ripoti hizo zinaonyesha katika kipindi cha miongo kadhaa iliyopita maambukizi hayo yanaongezeka na karibu robo tatu ya wakazi wake wana virusi vya ukimwi na ukimwi wenyewe.

Ili kupunguza athari za matatizo hayo, hivi karibuni Shirika la Umoja wa Mataifa la Ukimwi (UNAIDS) lilipendekeza kuanza kutumika kwa dawa mpya ambayo inaweza kuboresha afya ya mgonjwa.

Katika eneo la Afrika Mashariki, Kenya imekuwa nchi ya kwanza Barani Afrika kuanza kutumia vidonge vya ugonjwa wa ukimwi ambavyo vinaweza kuboresha afya na kurefusha maisha ya maelfu ya watu wanaosumbuliwa na maradhi nyemelezi ambayo hayakubali tiba nyingine.

Jina la dawa hiyo kitaalamu inatambulika Dolutegravir (DTG), lakini hujulikana kwa jina la Tivicay na inazalishwa na ViiV Healthcare, kampuni ambayo sehemu kubwa ya hisa zake zinamilikiwa na GlaxoSmithKline.

DTG imekuwa dawa ambayo ni chaguo la kwanza la watu wanaoishi na VVU kwa miaka miwili iliyopita katika nchi za watu wenye kipato kikubwa kwa kuwa ina athari chache, ni rahisi kutumia kuliko dawa za ARV zinazotumika sasa (yaani kidonge kimoja kidogo kila siku).

Kwa kutumia dawa hiyo, kuna uwezekano mdogo kwa wagonjwa kutengeneza usugu, kwa mujibu wa tovuti ya unitaid.eu. Mwaka 2015, Shirika la Afya Duniani (WHO) lilipendekeza DTG iwe chaguo la kwanza kwa watu wazima na vijana, lakini hadi siku za karibuni watu wanaoishi na VVU katika nchi kama Kenya walikuwa hawawezi kupata dawa hizo.

Vidonge hivyo ambavyo vilipitishwa kutumika nchini Marekani mwaka 2013, sasa vinagawiwa kwa wagonjwa 20,000 nchini Kenya kabla ya kupelekwa Nigeria na baadaye Uganda, kwa kusaidiwa na Unitaid, ambao ni wakala wa afya.

DTG ni dawa inayotumiwa na watu wenye VVU ambao hawakuwahi kutumia dawa za kufubaza makali ya Ukimwi (ARV). “Nilikuwa na tatizo la mara kwa mara la kutokuwa na hamu ya kula,” alisema mkazi wa Nairobi, Doughtiest Ogutu alipozungumza na taasisi ya Reuters Foundation.

Ogutu alianza kutumia dawa hizo mwaka huu kwa sababu tiba nyingine hazikuwa zinamfaa.

“Hamu yangu ya kula imerejea, mwili wangu unafanya kazi vizuri,” anasimulia.

Ogutu, ambaye ameishi na VVU kwa miaka 15, alisema kiwango cha VVU mwilini mwake kimepungua kwa kiasi kikubwa kutoka virusi 450,000 hadi 40,000 tangu aanze kutumia DTG.

Shirika la Unaids linalenga kuwa asilimia 90 ya watu watakaogundulika kuwa na VVU wawe wamepata dawa hiyo ifikapo mwaka 2020.