Wajawazito visiwa vya Ziwa Nyasa wanavyokumbana na adha ya huduma

Muktasari:

  • Wilayani Ludewa licha ya kufanikiwa kupunguza vifo vya wajawazito lakini hali bado tete kwa upande wa vifo vya watoto wachanga.

Bado kuna changamoto mbalimbali za upatikanaji wa huduma za uzazi salama, vifaatiba, dawa pamoja na wahudumu wa afya kwa wananchi wanaoishi visiwa vilivyo ndani ya Ziwa Nyasa.

Wilayani Ludewa licha ya kufanikiwa kupunguza vifo vya wajawazito lakini hali bado tete kwa upande wa vifo vya watoto wachanga.

Hivyo mikakati maalumu inahitajika ili kunusuru maisha ya watoto hao na mama zao.

Violeth Baraka (33) mkazi wa Kilondo Wilaya ya Ludewa anasema hatasahau aliponusurika kupoteza maisha wakati akiwahishwa hospitali ya Matema kujifungua, kwasababu alipatwa na uchungu mkali na akaanza kutokwa damu nyingi.

Hivyo mumewe ambaye ni mfanyabiashara wa vifaa vya umeme alilazimika kutafuta boti ya kukodi bila mafanikio.

Anasema ingawa alikuwa kwenye maumivu makali, alishuhudia mumewe alivyokuwa akipambana kuokoa maisha yake na ya mtoto wao mtarajiwa bila mafanikio.

Anasema kuna wakati mmewe alitokwa na chozi baada ya kujibiwa na mmiliki wa boti kuwa haitaweza kumsafirisha hata alipojaribu kuongeza mara mbili ya kiwango cha fedha za ukodishaji ambazo wakodishaji hutoza.

“Ilikua siku ngumu sana kwetu nililazimika kupanda mtumbwi, mume wangu alinilaza kifuani kwake huku akiniombea na kunifariji kuwa Mungu atanisaidia mimi na mtoto wetu tutapona na kadri muda ulivyozidi kwenda, hali yangu ilibadilika na nikapoteza matumaini ya kuishi hivyo nilijiombea kifo chema,” anasema Violeth

Anasema alishtuka akiwa ameshafika hospitali ya Matema na anachokumbuka aliambiwa pole na muuguzi kwa kupoteza watoto wake mapacha.

Mama huyo anasema aliumia zaidi baada ya kubaini kuwa amepoteza watoto wake kwa kukosa matibabu. “Nikasema labda ningewaokoa wanangu kama kungekuwa na hospitali yenye wataalamu na vifaatiba vya kutosha kama ilivyo hospitali ya Matema,” anasema.

Mama huyo ameiomba Serikali iwasaidia wananchi wanaoishi visiwani kwa sababu wamechoka kushuhudia watoto wao wachanga wakifariki dunia mama zao wanapojifungua.

Hata hivyo, mkazi mwingine wa eneo hilo, Sada Haule anasema changamoto kubwa ni uhaba wa wakunga.

Anasema wajawazito wengi wanajikuta wakijifungulia nyumbani na wengine hulazimika kusafiri umbali mrefu kwenda Ludewa mjini au Mbeya kujisubiria wajifungue kwasababu tu maeneo wanayoishi hayana wakunga wa kutosha kwenye vituo vya afya.

Anajitolea mfano yeye binafsi kuwa amewahi kujifungulia kwenye mtumbwi alipokuwa akisafirishwa kupelekwa hospitali kujifungua.

Naweza kusema ilikua ni bahati yangu tu nilimpata mwanangu Joseph nikiwa njiani narudi kutoka harusini, muda wangu wa kujifungua ulikua bado mimba ilikuwa na miezi saba. Nikapatwa na uchungu njiani, baada ya kujifungua nilirudi nyumbani na kumtunza njiti wangu kienyeji,” anasema Sada.

Kiongozi wa Serikali

Ofisa mtendaji wa kata ya Lumbila, Lenatus Mpolo anasema tatizo la wajawazito kujifungulia ndani ya ziwa kutokana na kukosekana kwa huduma za uzazi katika maeneo mbalimbali katika eneo lake ni kubwa.

Anasema hali ni mbaya zaidi kwa wakazi wa visiwani ambao wajawazito wengi huhitaji kusafiri umbali mrefu wa kutumia boti za kukodi kufuata huduma.

Wajawazti hao hulazimika kulipa nauli ya Sh120,000 na kama haipo hulazimika kukodi usafiri wa mitumbwi wanayolipia Sh40,000 hadi Sh55,000 pamoja na kumlipa mpalazaji (mpiga kasia).

Na kama ndugu wa mgonjwa wataambatana na mgonjwa nao hulazimishwa kusaidia kupika kasia ili chombo kiende.

“Hakuna boti ya Serikali, wananchi wanahitaji kulipia boti ya kukodi ambayo inatumia saa mbili kufika nchi kavu iliko hospitali ya misheni ya Matema iliyopo Kyela na kama watatumia mtumbwi wanasafiri kwa saa sita,” anasema Mpolo.

Mkakati wa kunusuru adha hiyo

Ofisa mtendaji huyo anasema tayari wameshapanga mkakati wa kuanza kuwahamasisha waja wazito kuhudhuria kliniki mapema.

“Tunafanya hivi kusudi wenye matatizo tuwabaini mapema na tuanze kuandaa mazingira ya kuwasafirisha kabla mambo hayajaharibika,” anasema Mpolo.

Anasema, mfano katika kata yake ya Lumbila, mjamzito anatakiwa asafiri umbali wa kilomita 100 kwenda kupatiwa matibabu

Mkakati wa mkoa

Ili kutatua changamoto ya vifo vya watoto wachanga wilaya ya Ludewa, mkoa wa Njombe, umeweka mikakati mbalimbali ya kuondoa vifo hivyo baada ya kufanikiwa kupunguza vifo vya wajawazito .

Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya Ludewa, Ng’wilabuzuu Ludigija anasema tangu Januari hadi Desemba, 2017, vifo vitokanavyo na uzazi ni vinne kwa wajawazito na 31 kwa watoto wachanga.

Anasema halmashauri yao inampango wa kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi kwa kuendelea kuutoa elimu kwa watumishi wa ukanda wa mwambao juu ya huduma za dharura kwa wajawazito na watoto wachanga.

“Kukamilisha ujenzi wa vituo vya afya vya vijiji vya ndani ya ziwa na pwani kwa kuanza kutoa huduma za afya ya uzazi salama karibu na jamii. Pia tunatarajia kukamilisha ujenzi wa zahanati ya Chanjale,” anasema.

Anasema tayari wameanza uhamasishaji kwa jamii wa kuwajengea uelewa juu ya huduma za afya ya uzazi salama kwa lengo kutambua viashiria vya hatari na kuhakikisha mjamzito anahudhuria kliniki kipindi chote na kwa wakati.

Hata hivyo, taarifa ya wilaya inaonyesha tangu Januri hadi Desemba mwaka jana, hakuna vifo vilivyotokea kwa kusababishwa na uzazi.

Isipokuwa changamoto ipo kwenye uchelewaji wa wajawazito kufika vituo vya afya kupatiwa huduma.

“Tumeanza ujenzi wa vituo vya afya katika kata za Lumbila, Kilondo na Lifuma. Ujenzi wa vituo hivi vyote upo hatua ya msingi,” anasema mkurugenzi huyo.

Amevitaja vituo vya tiba vilivyopo ukanda wa Ziwa Nyasa kuwa ni vya Kata ya Kilinzoni kuliko na zahanati yenye watumishi wawili .

Anasema inatoa huduma za CTC, RCH na OPD.

Kijiji cha Lumbila katika kata ya Lumbila kuna zahanati moja inayofanya kazi inayotoa huduma za CTC, RTH na OPD. Kituo hiki kwa mujibu wa mkurugenzi huyo kinahitaji ukarabati mkubwa.

Nyingine ni ya kijiji cha Chanjale inayotoa huduma ya OPD na ina mtumishi mmoja.

Mkuu wa Wilaya ya Ludewa, Andrea Tsere anasema pamoja na kufanikiwa kupunguza vifo vya wajawazito bado wanakazi kubwa ya kuondoa au kuzuia vifo vya mama na mtoto.

Tsere anasema awali tatizo lilikua kubwa zaidi hali iliyowalazimu kujipangia mkakati wa muda mrefu na mfupi ili kunusuru maisha ya wajawazito na watoto.

Anasema wengi walikuwa wakiugua hawaendi hospitali kutokana na umbali na kuamua kwenda kwa waganga kupata mitishamba wakiamini ni maradhi ya kurogwa.

“Tumejipanga kuhakikisha adha hii inamalizika kwa kuwabana wazazi wawapeleka watoto wao kliniki na tumeandaa daftari la orodha ya watoto wachanga wenye umri chini ya miaka mitano na wapo kinamama tuliowaweka wawafuatilie watoto wote wanaozaliwa kama wanapelekwa kliniki,” anasema mkuu huyo wa wilaya.

Anasema zaidi 26 na vituo vya afya saba vimeanza kujengwa katika kata mbalimbali wilayani humo na ujenzi uko katika hatua mbalimbali.

“Naamini vikikamilika vitasaidia sana kupunguza tatizo la upatikanaji wa huduma ya afya kwa mama na mtoto,” anasema Tsere.