Walemavu wa akili na ombaomba waongezeka London

Sunday September 16 2018Freddy Macha

Freddy Macha 

Unasubiri magari yapite.

Mbele yako jamaa wawili wanarushiana maneno na mateke. Wameshikana shingo.

Mashati yameshachanika chanika sasa kilichobaki kurarua raruana makucha. Mrefu zaidi, Mzungu, kazidiwa nguvu akaangushwa chini na mguu wake mmoja umebakia barabarani utadhani gongo la mti. Gari linapiga honi. Mwenzake mfupi, Mweusi, ana furukuta akitukana Kiingereza chenye lafidhi ya visiwa vya Karibian.

Ingawa uko mita hamsini mbali unaihisi ile chuki yao.

Wapita njia za miguu tunaangalia tukihofia na kustaajabu.

Wewe umetoka nyumba ya Mama Sara- kufundisha wanawe, Piano. Wazazi, Uzunguni hupenda watoto wafahamu muziki.

Kidesturi muziki ni sanaa ndiyo ila... hutumia mahesabu, kumbukumbu, mpangilio wa sauti, utunzi wa maneno na melodi, na kutuliza mitafaruku ya kisaikolojia. Muziki pia huwapa watoto jambo la kufanya na kuepuka tafrani za kujiunga na makundi ya kihuni au dawa za kulevya hasa wanapoingia sekondari.

Kisaikolojia muziki ni mzuri kwa wazee na watu wa makamo. Hujenga furaha moyoni na kuufanya ubongo usilemae. Kwa walemavu wa akili muziki waweza rejesha hisia zilizoharibika.

Baada ya kuwafundisha Sara na Michael, mapacha wawili wa miaka kumi, unaelekea soko bomba ukanunue kitoweo.

Ulikuwa ukisubiri taa zibadilike rangi kijani ndipo ukashuhudia kasheshe.

Hapa ulipo mtaa wa Edmonton, kaskaz ya Londonni njia panda yenye barabara nyingi zinazopishana.

Kila siku yupo msela mmoja mwenye kichwa kidogo chenye vijinywele vifupi vya matuta matuta kama vitunguu.

“Zamani alikuwa mwanamuziki,” alikueleza Mama Sara ulipomsaili . “Alikuwa mwimbaji safi. Na gitaa na bendi yake...mambo hayakumwendea vizuri. Bangi nyingi. Akaheuka...”

Kibarange. Mweusi tititi. Huvamia kila gari linalopita pale. Alipachagua kweli kweli. Hakuna omba omba mwingine anayeruhusiwa hapa. Ni kama benki. Magari husimama kila dakika tatu kusubiri taa. Na hapo Bw Rasta Kitunguu hutegea kuchuma. Atagonga kila kioo, kama akidai haki yake.

“Saidia maskini. Nyinyi wenye hela. Saidieni....”

Humaka Kiingereza.

Kawaida kazi ya muziki Ulaya si tu kupiga madensi.

Ukitegemea hivyo tu, utadata. Wanamuziki wengi huwa na kazi za mishahara huku wakitumbuiza muziki kama ajira ya pembeni. Wale walio na fani hii kama kazi mahsusi, hufundisha (kama wewe unavyofanya ) au kuendesha warsha ndefu zenye malipo mazuri. Yaelekea mwenzetu Kitunguu hakufuata utaratibu huu.

Mara moja moja utamwona na gitaa lake. Mwepesi kutukana kila mtu.

“Nyinyi wote wachoyo tu! Jehanam itawachoma!”

Kama tulivyosema hakuna omba omba mwingine anayeruhusiwa eneo hili. Yupo mmoja mathalani kajenga kambi, nyuma ya soko bomba unaloelekea. Ana kajigodoro na shuka zilizoshachakaa chakaa, makasha na makabrasha yenye nguo zilizosokotana sokotana na kukukunjana kunjana; bakuli, kikombe na sahani, chupa za pombe na sigara. Mzungu.

Tunaelezwa alitoka nchi iliyokuwa na vita, Mashariki ya Ulaya, miaka kumi iliyopita. Ukraine au Kosovo.

Sasa leo alipomwona Rasta Kitunguu hayupo akaelekea ilipo njia panda ya magari.

Ugomvi wa hawa omba omba unakukumbusha bondia Hassan Mwakinyo alivyomtwanga Mwingereza Sam Eggington. Ila huu si mchezo wa malipo. Ni dunia tambara bovu la omba omba wa mitaa ya London.

Tuendelee wiki ijayo...

Advertisement