Wanaotufanya tuzidi kumwombea Ruge

Hii kwangu hutokea mara chache. Kulipuka pamba mpaka nikajihusudu. Katika mara chache hizo hii ilikuwa mojawapo. Achilia mbali kuvaa, muda wa kuzurura madukani kutafuta pamba haupo. Majukumu yamekuwa mengi kuliko wadudu wa malaria.

Siku hiyo nililipuka mpaka mimi mwenyewe nikajitamani niwe mimi, halafu mimi mwingine niwe kando yangu nikijitazama mimi. Sikumbuki sababu ya kulipuka pamba namna ile. Haikuwa weekend, sikukuu wala birthday. Niliamua tu kwenda sawa na mabishoo.

Dawa ya mabishoo kuwa bishoo zaidi yao. Nilikuwa bishoo kuliko ubishoo wenyewe. Kwanza mfukoni nilikuwa mtamu. Uchakavu ulivimbisha ‘waleti’ kiasi kwamba utawala huu ungenigundua ningewekwa kundi la malaika wanaostahili kuishi kama mashetani.

Ogopa sana mtu mwenye mkwanja wa kutosha maeneo ya bata. ‘Fulu’ kujiamini. Naagiza nitakacho na kutoa ofa nitakavyo. Ghafla kujiamini kwangu kulipungua baada ya macho kutuama kwenye mwili wa kiumbe wa kike mbele yangu. Mapigo ya moyo yaliongezeka kwa kasi sana.

Moja ya vipaji nilivyojaaliwa na Mungu, ni uwezo wa kutambua totozi nzuri. Hii totozi sikuhitaji sekunde mbili kujua kama ni nzuri. Macho yalipomuona yakawasiliana na ubongo, moyo, mapafu, figo, bandana mpaka maini. Ndani ya sekunde moja yakathibitisha kuwa mrembo bora kasimama mbele yangu.

Nilipenda pozi zake, ngozi na kimo chake. Zaidi nilivutiwa na tabasamu lake ambalo kwa wajuvi wa mambo kama sisi huliita ‘shirikishi’. Yaani tabasamu ambalo hupingana na mishipa ya taya kutanua mdomo. Akicheka kama hataki. Kamtazame Michelle Obama naye akitabasamu yuko namna hiyo.

Macho na mawazo yakahamia kwake. Kujiamini kukapungua kama vile niko kizimbani kwa kesi ya utakatishaji fedha. Utulivu wangu ukagundulika na kila aliyekuwa jirani yangu. Mpaka mhudumu akacheka akinitazama. Cheko lake halikuweza kuihamisha akili yangu kwa kiumbe huyu. Nilizubaa kibwege sana.

Mshikaji niliyekuwa naye, alinitonya jina la mrembo huyo na shughuli zake. Hapo ndipo akili ikarudi mezani nilipokaa. Yalikuwa maeneo ya Kawe kwenye baa moja maarufu sana. Ndipo nikamuona kiumbe huyu akiwa na kampani yake, bahati mbaya hawakuwa wazuri kama yeye.

“Kumbe mzuri kuliko nyimbo zake?” Nilijiuliza kimoyomoyo baada ya kujulishwa jina. Lulu Diva ni maarufu lakini si wa daraja la Jide au Vanessa Mdee, kwamba ukimuona tu mara moja utamtambua. Hapana, huyu ni toleo la mastaa wa kike waliotoka ghafla kwa mkupuo.

Huyu ni kati ya wale wasichana wa mjini ambao sura zao nzuri, maumbo yao matamu na kujichanganya kwao kuliwakutanisha na watu na kuanza kupata ‘dili’ za kupamba video za wanamuziki. Baada ya kufanya video mbili tatu, nao wanapata umaarufu na njia za kutoka kimuziki.

Hakuanzia kwenye filamu kama Shilole au Snura. Isingekuwa rahisi kumtambua haraka. Lulu Diva ni aina ya wale ambao unaanza kumpenda yeye kabla ya kazi yake. Hapo kabla sikuzingatia, baada ya siku ile kazi zake nasikiliza na kutazama sana. Sababu ni ule mvuto wake binafsi wa shepu na sura.

Sasa hilo kundi la wasichana wapambaji wa nyimbo za wanamuziki, nao wameamua kufanya muziki. Yawezekana ni kusaka maslahi makubwa au pengine baada ya kugundua kuwa muziki ni jambo dogo ukiwa na mvuto wa sura na umbo. Sasa ni dunia ya mvuto, dunia ya vipaji inatoweka.

Giggy Money na Amber Lulu walianza kama video vixen. Sasa tunalazimika kuwaita mastaa wa muziki. Ndivyo ilivyo kwa Lulu Diva; kabla ya kupiga shoo za Fiesta alikuwa mpambaji wa nyimbo za kina Ney Wa Mitego. Wanapanda chati kutoka video vixen, mpenzi wa mwanamuziki kisha mwanamuziki.

Hawa wasichana siwalaumu. Kinachotokea ni kwamba wanaangalia muziki wa wanamuziki wetu. Wanaona kabisa uwepo wao kwenye video umeongeza mvuto wa wimbo kuliko shairi na midundo yake. Kwa nini wasifanye wao na kuanika mapaja yao kwenye video wapate mashabiki? Ndicho kinachotokea sasa.

Kwenye filamu ilianza namna hii. Soko lao lilipokuwa juu likaanza kulazimisha mvuto kuwa juu ya kipaji. Kila demu mwenye mvuto mjini akageuzwa staa wa filamu na kina Kanumba. Vipaji vikatengwa na dunia ya filamu kisha filamu zikafunga ndoa na mamiss na wanamitindo.

Bongo Movie yote ilijaa ‘mabrazameni’ wa kumwaga na ‘masista duu’ wa kutosha. Kama huna mvuto huna chako. Vipaji peleka Bagamoyo, siyo kwenye sanaa ya filamu. Game likapinduka waigizaji hao hao wakageukia muziki baada soko la filamu kuporomoka.

Mademu walioshirikishwa kwenye filamu na kulipwa kwa ‘sini’ nao wakaona kama wana mvuto kwa jamii kwa nini wasitengeneze filamu zao? Kama video vixen kugeuka wanamuziki. Waigizaji nao wakageuka ‘madairekta’ na kuanza kutoa filamu zao wenyewe. Shughuli ikaishia hapo.

Shilole ni mwanamuziki siyo muigizaji tena. Snura kasahau hata marafiki zake wa filamu kajikita kwenye muziki. Wema naye aliwahi kubahatisha kutoa wimbo na Snura. Bila shaka akajipima akagundua hatoshi, akaamua kukaa kando. Jokate pia aliwahi kutaka kujikita kwenye muziki.

Siyo hawa tu. Kipindi anatoka kimuziki Jide, watangazaji wengi wa kike waligeukia muziki. Hawa kina Vanessa Mdee ni muendelezo wa watangazaji wa redio waliotamani kushika maiki majukwaani. Sasa leo hata Nisha wa Bongo Movie anataka tumuite mwanamuziki.

Licha ya uvamizi wa mademu wa filamu na wenye mvuto tu mjini kwenye muziki, watu kama Ruge Mutahaba walitumia nguvu na vipawa vyao kusimamisha vipaji kwenye muziki badala ya wasichana wenye mvuto. Ndiyo kina Ruby na Nandy walipoibuliwa na kukimbiza sana kwenye game.

Wakati ule kila msichana akitamani kuwa muigizaji, kina Ruge wakawashika mkono kina Mwasiti, Linnah na wenzao wengi tu na maisha yakawa matamu kupitia muziki. Hivi sasa tunaambiwa mvuto wa Mobetto unataka kugawana keki na kipaji cha Nandy.

Achana na Hamisa Mobetto, kuna video vixen mwingine anaitwa Lynn naye katoa wimbo. Kuna mwingine wa kuitwa Kimnana naye anataka kutoa wimbo agawane keki na Ruby. Wamechoka kupamba video za watu wanataka kuimba wao.

Ukitaka kujua mvuto wa kike unakomba keki ya vipaji vya kike kwenye muziki, tazama majukwaa makubwa kama Fiesta, Muziki Mnene na Wasafi Festival. Kwenye ‘listi’ wamejaa waliongia kwenye muziki kwa mvuto siyo vipaji. Ndivyo ilivyokuwa Bongo Movie kabla ya umauti wa soko lao.

Tatizo ni wanamuziki wenyewe kutuaminisha kuwa video nzuri ni yenye warembo wengi. Waliovaa na kucheza kihasara. Na watazamaji wa YouTube wanapenda haya mambo yanayowaongezea views wanamuziki na kupiga chapaa za YouTube.

Mobetto anategemea wafuasi wake mtandaoni ambao wanapokea kitu chake chochote; kiwe kizuri au kibaya. Anapata views anapiga pesa za YouTube.

Tunaukosea heshima muziki kumbeba Mobetto na kumpuuza Vumilia. Kuamini katika Lulu Diva na kumkwepa Grace Matata. Tunataka Mwasiti aombe shoo kwa Amber Lulu au Gigy Money? Tunajaribu kuishi kinafiki kwa kuamini Snura ni zaidi ya Ruby?

Mazingira hatarishi kwa vipaji tunalazimika kumuombea sana Ruge arudi kwenye afya yake. Mtu anayesimamia vipaji halisi miaka nenda rudi. Muda mfupi akiwa kitandani huku vipaji halisi vinatengwa tukiaminishwa kwenye mvuto wa sura na maumbo.