Wanigeria wanatoboa kwetu kwa sababu tumetaka wenyewe

Muktasari:

  • Waliokuwa wanapinga wanasema wametembea nchi nyingi duniani lakini wanapofika katika kumbi za starehe nyimbo wanazosikia ni zile za Afrika Magharibi hasa Nigeria.

Juzi kati nilikuta mabishano makali juu ya muziki wa Bongo Fleva. Mada mezani ilihusu madai kuwa muziki huo umetoboa mipaka ya anga la Tanzania kwamba sasa unasikilizwa nchi nyingi duniani.

Waliokuwa wanapinga wanasema wametembea nchi nyingi duniani lakini wanapofika katika kumbi za starehe nyimbo wanazosikia ni zile za Afrika Magharibi hasa Nigeria.

Wengine walitetea wakisema muziki wa Nigeria unapigwa kutokana na wingi wa watu hao katika mataifa mbali mbali duniani.

Yaani DJ hawezi kupiga Bongo Fleva mfululizo katika klabu ya usiku nchini Uingereza wakati kuna Watanzania wawili tu.

Anayebisha kwamba Bongo Fleva haijapenya alipinga utetezi huo kwa hoja kwamba mbona hata hapa kwetu nyimbo za Nigeria zinapigwa sana kuliko Bongo Fleva ina maana Wanigeria ni wengi kuliko Watanzania hapa pia? Mimi binafsi niliona jamaa ana hoja katika hili. Leo hii wasanii nchini hawashindani wenyewe kwa wenyewe bali mpinzani wao ni Mnigeria na ndio maana kinachowatofautisha ni lugha tu.

Hivi wakati Lingala (muziki wa Congo) inatamba Afrika raia wa nchi hiyo walikuwa wengi tofauti na sasa? Vipi kuhusu Kwaito nayo je, raia wa Afrika Kusini wamepungua sasa? Wasanii wamekuwa watumwa wa Nigeria. Ni kweli nchi hiyo inaitawala Tanzania (siwezi kusema Afrika kwa sababu sina uhakika kama nchi nyingine zinawaendekeza kama sisi).

Hata mwanafunzi darasani akipewa mtihani wa kutaja majina 10 ya wasanii anaowafahamu huenda saba kati ya hao ni Wanigeria.

Siyo mbaya kwa kuwa tunaamini ni muziki mzuri lakini swali ni je, tunauweka wapi muziki wetu? Kwa nini usiwepo utaratibu wa kuhakikisha asilimia 80 ya muziki unaopigwa klabu, redioni au televisheni ni wa nyumbani.

Wanigeria wamewekeza kwenye muziki ndio maana wanaitawala Afrika kitu ambacho hata sisi tunaweza kuamua kukifanya, lakini tumeamua kuwafuata kama vile na sisi ni wao. Muziki wetu unaendeshwa na mipango ya Wanigeria. Wakisema muziki ni video na sisi tunafuata mkumbo. Wakiamua muziki ni midundo fulani utaisikia kwenye nyimbo zetu zote.

Kupanga ni kuchagua. Mimi nakubaliana na aliyesema muziki wetu kutoboa bado sana kwa sababu hata kama unasikilizwa huko bado baadhi hauwatofautishi na wao kwa sababu kwa haraka haraka msikilizaji anaweza kuhisi ni mwenzao.