Wapinzani, wanaharakati wahofu kurejeshwa mfumo wa chama kimoja

Muktasari:

  • 1965 ni Mwaka ambao mfumo wa vyama vingi vya siasa nchini uli-futwa na kubakia chama kimoja cha Tanu kilicho-shika hatamu za uongozi wa nchi.
  • 1992 Ni mwaka ambao Tanzania ilirejea kwenye mfumo wa demokrasia ya vyama vingi vya siasa.

“Si uhaini kujadili mfumo wa vyama vingi. Ukiona mwenzio ananyolewa na wewe tia maji.” Ilikuwa ni kauli ya Mwalimu Nyerere wakati Tanzania ikiwa kwenye shinikizo la kuruhusu mfumo wa vyama vingi vya siasa.

Mwalimu hakuishia hapo kuna wakati aliwahi kutamka: “Hatuwezi kutumia sababu za mwaka 1965 kukataa mfumo wa vyama vingi mwaka 1990.”

Ni miaka 26 sasa tangu Tanzania iruhusu demokrasia ya mfumo wa vyama vingi vya siasa, Rais wa awamu ya pili Ali Hassan Mwinyi aliuonja mfumo huo kwa chaguzi ndogo za ubunge katika jimbo la Ileje mkoani Mbeya na Kwahani visiwani Zanzibar.

Mbali na changamoto zingine za kidemokrasia, tangu kuanzishwa kwa mfumo wa vyama vingi utendaji wa Serikali ya CCM nao ulibadilika.

Demokrasia ndani ya chama ilizidi kupungua na hasa nafasi za viongozi zilikwenda kwa walewale ambao walijulikana kama ‘mwenzetu, kijana wetu na ndugu yetu.’ Kwa ujumla chama kilibweteka. Ndio sababu ya Mwalimu Nyerere kusema kuwa mfumo wa vyama vingi hukifanya chama kilichopo madarakani kisibweteke.

Mageuzi ya kisiasa

Tangu uchaguzi wa kwanza ufanyike baada ya kurejeshwa kwa mfumo huo mwaka 1995, CCM imekuwa ikivishinda vyama vya upinzani kwa mbali, jambo linaloelezwa kuchangiwa na mfumo unaokibeba ikiwa pamoja na Katiba ya Jamhuri ya Muungano.

Licha ya CCM kubebwa na mfumo huo, awamu ya tano chini ya Rais John Magufuli iliyoingia Novemba 2015 imetajwa kuweka vikwazo zaidi kwa vyama vya upinzani kutokana na matamko mbalimbali na sasa mabadiliko ya Sheria ya vyama vya siasa ya mwaka 1992, pia kuwasilishwa bungeni muswada wa mabadiliko ya sheria ya vyama vya siasa.

Muswada huo unaolenga kuirekebisha sheria hiyo siyo tu umewapa hofu vyama vya upinzani wa kushindwa uchaguzi, bali pia umewapa hofu wadau wa demokrasia ya vyama vingi.

Hivi karibuni, baadhi ya makada na wanaharakati wa haki za binadamu wamekutana kwenye kongamano la haki za binadamu lililoandaliwa na Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) hivi karibuni jijini Dar es Salaam na kupaza sauti zao dhidi ya sheria hiyo.

Mbunge wa Ubungo, Saed Kubenea anasema muswada huo haukupaswa hata kuingia bungeni na kwamba kuingia kwake kumeonyesha udhaifu wa Bunge.

“Sisi Wabunge ndiyo watu wa aibu kabisa, tuko bungeni tunatoka nje tunaanza kulalamika hii sheria mbaya. Tuna wajibu wa kuchukua hatua. Tunayo mamlaka ya kikatiba ya kumwondoa Rais madarakani,” anasema Kubenea.

Sasa muswada unakuja bungeni tunaupitisha, haki zetu sisi kama wabunge za matangazo yetu, hotuba zetu kwa wananchi hazitoki, tuko pale tunanyamaza.

Shida yetu kubwa tunalalamika sana lakini hatuchukui hatua,” anaongeza.

Kubenea anasisitiza licha ya vikwazo vingi wanavyopata wapinzani bado wanaweza kupiga kelele na kuleta mabadiliko.

Kauli ya Kubenea iliungwa mkono na Mbunge wa Moshi Vijijini, Anthony Komu aliyekumbusha harakati za mageuzi mwishoni mwa miaka ya 1980 alipokuwa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

Anasema tangu awali siasa za vyama vingi zilipigwa vita lakini walipambana na kuleta mabadiliko.

“Mwaka 1965 aliyekuwa Balozi wa Tanzania nchini Uingereza, Kasanga Tumbo alirudi Tanzania na kupinga mfumo wa chama kimoja akaitisha mkutano kueleza. Aliwekwa kizuizini wilayani Sikonge mkoani Tabora hadi mwaka 1989 Mwalimu Nyerere aliposema atoke. Tukamfuata Sikonge tukamleta Dar es Salaam,” alisema Komu.

Aliwataja pia wanaharakati wengine wa siasa wakati huo akiwemo James Mapalala akisema walipelekwa vizuizini wakati wa Mwalimu Nyerere kwa kutaka mageuzi ya kisiasa.

Kwa upande wake Ismail Jussa kutoka CUF Zanzibar naye anakumbusha mapambano yaliyoleta upinzani Zanzibar akisema mapambano hayo ndiyo yatakayoondoa sheria kandamizi.

“Mabadiliko hayaji kwenye sinia, lazima uyapiganie. Watu wamefungwa watu wamekufa. Wamekuwa wakiimba CCM ni ileile, ni ileile kweli. Chuma kikipitishwa kwenye moto. Mapambano haya hayataletwa na mtu mmoja, hayataletwa na Zitto au na Maalim Seif. Lazima tusimame tumwambie Mutungi (Jaji Francis) kuwa hatutaki mfumo wa chama kimoja,” anasema Jussa.

Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu kilichoandaa kongamano hilo kimesema kiko tayari kuvisaidia vyama vya upinzani kisheria kupinga marekebisho ya sheria ya vyama vya siasa inayokusudiwa kupelekwa bungeni siku za usoni.

Akizungumza katika kongamano la haki za binadamu lililofanyika jijini Dar es Salaam, Mwanasheria wa LHRC, Raymond Kanegene akisema wako tayari kuwapa msaada vyama hivyo watakapofuatwa.

“Sisi kazi yetu ni kutoa technical support (msaada wa kiufundi) jinsi ya kupinga hiyo sheria, kwa hiyo wakija tutawasaidia,” anasema Kanegene.

Kanegene anasema marekebisho hayo ni mwendelezo wa sheria mbovu zilizotungwa katika kipindi kifupi ikiwa pamoja na Sheria ya makosa ya mtandao, Kanuni za Sumatra za kutojadili siasa kwenye gari na sheria ya upatikanaji wa sheria.

“Sheria yenyewe ina vifungu 22, marekebisho yapo vifungu32. Katiba yetu, tamko la Haki za binadamu vinaendana na sheria hiyo?” anahoji.

Hata hivyo, akizungumza na Mwananchi katika mahojiano maalum jijini Dar es Salaam, Msajili msaidizi wa vyama vya siasa nchini, Sisty Nyahoza amesema vyama vyote vya siasa vilishirikishwa kwenye maandalizi ya muswada ambao sasa wanaulalamikia.

“Huu mchakato wa marekebisho ya sheria ya vyama vya siasa, haukuanza leo, bali ulinza mwaka 2013. Mwaka huo tuliita kongamano la wadau pale ukumbi wa Mwalimu Nyerere.

“Nashukuru kwamba wamekiri kwamba tuliwashirikisha, mambo yao mengi sana yameingia kwenye huu muswada,” alifafanua Nyahoza.