Watendaji serikalini wajitenge na migogoro

Muktasari:

  • Baadhi ya migogoro hii inachangiwa na watendaji wa Serikali wanaosimaia masilahi yao na kushindwa kufanya maamuzi sahihi.

Siku za karibuni migogoro inaongezeka katika maeneo mbalimbali nchini.

Baadhi ya migogoro hii inachangiwa na watendaji wa Serikali wanaosimaia masilahi yao na kushindwa kufanya maamuzi sahihi.

Kuna maeneo kuna migogoro baina ya wafanyabiashara na Mamlaka ya Kodi ya Mapato Tanzania (TRA), kuna migogoro baina ya wahifadhi na wananchi na pia kuna migogoro ya wakulima na wafugaji .

Ukiitazama baadhi ya migogoro unaona ingeweza kutatuliwa bila kuleta madhara, lakini ambacho kinaonekana kuna watendaji ambao ama kwa kujua au kutojua wanakuwa ni sehemu ya migogoro.

Mfano, suala la kuzuia uvuvi haramu na biashara ya samaki, wanaopata shida ni wananchi hasa masikini ambao hawamudu kwenda kununua kitoweo hicho kutoka nje ya nchi.

Hivi karibuni tumepata taarifa kupitia vyombo vya habari kuhusu zuio la kusafirisha samaki bila kuwa na vibali, hili sidhani kama lina masilahi mapana kwa taifa.

Udhibiti wa maeneo ya uvuvi ndio suluhu lakini sasa adhabu inawakumba wengi, suala ambalo sidhani kama ni suluhu ya tatizo.

Matokeo yake sasa samaki kutoka nje ya nchi, wameongezeka katika soko na pia bei ya samaki inaendelea kupanda. Sasa hapa tunamsaidia nani?

Hivyo wachache kwa nia zao ambazo hazijulikani wanataka kujenga chuki dhidi ya serikali kwa mambo ambayo yalipaswa kumalizwa kwa mazungumzo au kupuuzwa tu.

Vilevile katika maeneo kadhaa, kuna migogoro ya wafanyabiashara na maofisa wa TRA, yanayotokana na kudaiwa kodi kubwa na baadhi kufunga biashara.

Ingawa inajulikana wafanyabiashara mara zote wanapenda faida kubwa, lakini kuna wakati majadiliano ni muhimu ili kuzuia kuendelea kufungwa maduka na biashara mbalimbali.

Lakini, watendaji wachache kutaka kuonekana wao ni wazalendo au kutokana na hofu za kulinda vibarua vyao, sasa wanasababisha bidhaa kuendelea kupanda bei na nyingine kukosekana.

Kuna migogoro baina ya hifadhi za wanyamapori na wananchi, hapa tunashuhudia baadhi ya viongozi kwa masilahi yao hasa ya kisiasa wamekuwa sehemu ya migogoro.

Baadhi ya viongozi hawa wanashindwa kuwaeleza ukweli wananchi wanaovamia maeneo ya hifadhi au mapori ya akiba kuwa ni makosa kwa kuzingatia masilahi mapana ya taifa.

Lakini, hawa watendaji wamekuwa watetezi wa wahalifu hata kwa wale ambao wameanza kuchimba madini ndani ya hifadhi, jambo hili linachochea chuki baina ya wananchi na serikali.

Kumekuwapo na migogoro baina ya wakulima na wafugaji, hapa napo kuna mkono wa viongozi, kutokana na baadhi kumiliki ardhi kubwa ambayo haifanyiwi kazi. Ni muhimu viongozi wa Serikali watangulize masilahi mapana ya taifa katika maamuzi yao.

Watambue kwamba chuki binafsi haziwaathiri watu wachache ambao wamewadhamiria, bali zinasambaa maeneo mengi na hivyo mwisho wananchi wengi wanaathirika. Lakini, baadhi ya watendaji wa Serikali kama wakiendelea kujali masilahi yao wajue athari zake ni kubwa kuliko wanavyofikiri na mwisho huwarudia hata wao na familia zao. Tanzania ni yetu sote na hakika hakuna Mtanzania mwenye akili timamu ambaye hapendi maendeleo, amani na utulivu katika taifa lake.

Mussa Juma ni mwandishi mwandamizi wa Gazeti Mwananchi Mkoa Arusha