Watetezi walivyogeuka kuwa mwiba kwa Zuma, Mugabe

Muktasari:

Nimejifunza kwamba katika baadhi ya nchi maadui wa viongozi wa vyama tawala si viongozi wa upinzani, bali wafuasi kindakindaki ndani ya vyama vinavyotawala. Chama cha African National Congress (ANC) cha Afrika Kusini na Zanu-PF cha Zimbabwe ni mifano mizuri.

Mpenzi msomaji leo nakuletea mada kuhusu propaganda iliyotumika kwa miaka mingi na umoja wa vyama vya zamani vya ukombozi kusini mwa Afrika (FLMSA) kuaminisha watu kuhusu maadui wa viongozi.

Nimejifunza kwamba katika baadhi ya nchi maadui wa viongozi wa vyama tawala si viongozi wa upinzani, bali wafuasi kindakindaki ndani ya vyama vinavyotawala. Chama cha African National Congress (ANC) cha Afrika Kusini na Zanu-PF cha Zimbabwe ni mifano mizuri.

Yaliyowapata Zuma, Mugabe

Kwamba hadi Desemba 18, 2017, Jacob Zuma wa Afrika Kusini alikuwa na udhibiti mkubwa wa ANC lakini siku hiyo mara baada ya kuchaguliwa aliyekuwa naibu wake, Cyril Ramaphosa kukiongoza chama hicho, ghafla alipoteza uungwaji mkono na wafuasi wake wakaanza kumshinikiza ajiuzulu.

Vilevile hadi mwanzoni mwa Novemba 2017, Robert Mugabe alikuwa na mamlaka kama rais na kiongozi mkuu wa chama tawala cha Zanu-PF nchini Zimbabwe, lakini katika mabadiliko ya mawaziri aliyofanya ili kulipa nafasi kundi la G40 kuteua mrithi wake, alijikuta ametikisa hata jeshi la ulinzi. Novemba 15, 2017 Mkuu wa majeshi, Jenerali Constantion Chiwenga aliingiza mitaani vijana wake na kushika kwa muda mamlaka ya nchi na baadaye kumkabidhi madaraka aliyekuwa makamu wa rais, Emmerson Mnangagwa.

Kwa Afrika Kusini halikuwa tukio la ajabu kwani hiyo ndiyo njia aliyotumia Zuma kuingia ikulu baada ya kumpiga kumbo Thabo Mbeki. Kwa Zimbabwe, ilishangaza dunia kwani Mugabe alionekana kuwa mbuyu usiotikisika.

Viongozi wawili hao walijijengea wafuasi wengi na watetezi. Waliojitokeza kuchuana nao waliitwa wasaliti au vikaragosi na majina mengine.

Vyama vya ukombozi

Katika kipindi cha kuelekea mkutano wa umoja wa vyama vya zamani vya ukombozi kusini mwa Afrika (FLMSA) mwaka 2017, ANC ilishiriki kuandaa ripoti iliyojaa tuhuma, kwamba mabeberu wa Magharibi walikuwa wanashirikiana na vyama vya upinzani na asasi za kiraia ili kuwaondoa madarakani viongozi wao.

Walengwa wa kuondolewa madarakani, kwa mujibu wa ripoti ambayo ANC iliviambia vyombo vya habari, ni Zuma (Afrika Kusini) na Mugabe (Zimbabwe).

Propaganda nyingi zikapigwa (wapinzani wakaitwa wasaliti) kuonyesha mbinu zinazotumiwa na mabeberu hao ni kwamba mabeberu wanatumia watu kutengeneza mada kwenye kompyuta na simu (hashtag) zinazohusu kampeni chafu kama vile “Zuma Lazima Aondoke” ili kubadili utawala Afrika Kusini na nchi nyingine.

Ripoti hiyo iliyoandikwa juu “Siri” ilitaja vyama vya upinzani kama Renamo cha Msumbiji na Democratic Alliance (DA) na Economic Freedom Fighters (EFF) vya Afrika Kusini kama mfano wa nyenzo za mabeberu.

Tuhuma nyingine zilizotajwa katika ripoti hiyo ni kwamba nchi za Magharibi zinaanzisha vituo vya kijeshi katika ukanda huo kama maandalizi ya mabadiliko ya nguvu ikiwa njia nyepesi zitakuwa zimeshindwa.

Andiko hilo liliandaliwa kwa kuzingatia warsha ya makatibu wakuu wa nchi sita wanachama wa vyama vya zamani vya ukombozi kusini mwa Afrika akiwemo Katibu Mkuu wa ANC, Gwede Mantashe ambaye gazeti la The Standard lilimwelezea kama “mkuu wa nadharia ya njama” na kwamba masilahi ya Marekani na Uingereza ndiyo mkono unaojaribu kuchagiza mabadiliko ya utawala katika ukanda wa Kusini mwa Afrika.

Februari 2016, Mantashe alisema katika maandamano ya kupambana dhidi ya ubaguzi wa rangi, ANC ilikuwa inafahamu mikutano ya mara kwa mara katika ubalozi wa Marekani na vijana wa Afrika Kusini.

“Mikutano hii haina kingine chochote bali kuhamasisha mabadiliko ya utawala. Tunafahamu mpango wa kuchukua vijana kwenda Marekani kwa wiki sita, kuwarudisha na kuwapanga katika kampasi na kwingineko,” alisema.

Julai 2016, baada ya mkutano wa kamati tendaji ya kitaifa ya ANC, Mantashe aliwaambia waandishi wa habari kuwa maandamano nchini Zimbabwe na ukosefu wa utulivu wa kisiasa Msumbiji ilikuwa mifano ya “matukio yaliyofadhiliwa” yanayolenga kuleta mabadiliko ya serikali.

Alipoulizwa iwapo ANC iliamini kuwapo “njama za mabeberu” ili kukiondoa madarakani chama hicho pamoja na vyama vingine vya ukombozi katika ukanda huu, Mantashe alisema ripoti hiyo inawakilisha msimamo rasmi wa ANC.

“Tunakubaliana nayo. Sisi ni sehemu ya harakati za ukombozi. Nembo yetu iko katika ripoti. Inahusu vyama vya ukombozi na sisi tukiwamo,” alisema.

Hakupenda kuonyesha ikiwa alikuwa na ushahidi wa kuunga mkono madai hayo.

“Hiyo ni ripoti ya utafiti ... sio hati ya kiapo,” alisema na kuongeza: “Ikiwa huwezi kuziona ishara za njama za mabadiliko ya serikali nchini Afrika Kusini siwezi kukuwezesha uzione.”

Kwa Zimbabwe aliyekuwa mpiga debe wa siasa za kupakazia upinzani ni aliyekuwa Katibu wa utawala wa Zanu-PF, Ignatius Chombo. Kiongozi huyo ndiye alifafanua maazimio ya FLMSA yaliyofikiwa katika mkutano wa Novemba 2015 uliofanyika Msumbiji na wa Mei 2016 uliofanyika Victoria Falls, Zimbabwe.

Vyama vinavyotawala

Vyama wanachama wa FLMSA na ambavyo ndivyo vilivyobaki madarakani ni Zanu-PF, Swapo cha Namibia, Frelimo cha Msumbiji, MPLA cha Angola, ANC na Chama Cha Mapinduzi (CCM) cha Tanzania.

Chombo, ambaye wakati huo alikuwa Waziri wa Mambo ya Ndani nchini Zimbabwe, alielezea mpango wa FLMSA wenye hatua tisa uliolenga kuimarisha ushirikiano wao dhidi ya nguvu za upinzani zinazoongezeka katika kila nchi.

Moja ya hatua hizo ni vyama hivyo kuanzisha magazeti ya kila siku, vituo vya redio na televisheni na mitandao ya kijamii ya maana ili kusambaza propaganda zao na kukabili propaganda za upinzani.

Hii ndiyo sababu za kuwapo vyombo vya habari katika nchi mbalimbali vinavyoandika habari nyingi na nyingine za uzushi dhidi ya wapinzani na havichukuliwi hatua.

Hii ndiyo sababu wapinzani hunyimwa fursa za kujieleza kwa wananchi kama Katiba za nchi zinavyosema.

Hii ndiyo sababu wapinzani hushutumiwa pengine bila kuwepo ushahidi wowote kwamba wanatumiwa na mabeberu ili kuwaondoa madarakani viongozi wao.

Hii ndiyo sababu FLMSA imewaweka katika kapu moja, kundi la waasi wa Msumbiji (Renamo) na vyama vya DA na EFF vya Afrika Kusini.

Ukweli ulivyo

Propaganda hizi za FLMSA zimekuwa zikitumiwa kuficha moto uliomo ndani ya vyama hivyo na kusingizia vyama vya upinzani. Kutokana na juhudi kubwa za kupambana na upinzani wa nje yaani vyama vya upinzani, Zuma aliondolewa na kurithiwa na makamu wake, Cyril Ramaphosa na Mugabe aliondolewa na jeshi na nafasi yake kurithiwa na makamu wake, Emmerson Mnangagwa. Je, hao walitumiwa na mabeberu?

Ramaphosa alipata nguvu kutoka kwa wafuasi wa ANC waliomchoka Zuma, na Mnangagwa aliungwa mkono na jeshi na wafuasi wa Zanu-PF waliotaka utawala wa Mugabe uondolewe kwa amani. Je, tuamini mabeberu waliwatumia Ramaphosa na Mnangagwa?

Ingawa viongozi wa upinzani ndio waliokuwa wakishutumiwa Afrika Kusini na Zimbabwe, bado Zuma na Mugabe waliondolewa bila wapinzani hao kushiriki.

Wafuasi wa Zuma wanaondolewa mmoja baada ya mwingine wakati baadhi ya wafuasi wa Mugabe akiwamo Chombo aliyejiona mzalendo zaidi walikamatwa na kuwekwa ndani huku wengine akiwemo Jonathan Moyo wakikimbilia uhamishoni.

Haya yaliyotokea ndani ya ANC na Zanu-PF ni ushahidi wa wazi kwamba vyama vya ukombozi vinakabiliwa na upinzani usioonekana ndani yake huku vikisingizia upinzani kutumiwa na mabeberu.