Waziri Mpango anavyokuna kichwa kujibu hoja za Bajeti

Muktasari:

  • Zipo hoja kadhaa, zikiwamo tano zitakazomfanya waziri akune kichwa zaidi kuzipatia majibu kutokana na kujitokeza kwa wingi katika mjadala huo ambao unahitimisha kesho Jumatatu, ikiwamo ya Serikali kutotaka kurejesha asilimia 65 ya ushuru iliyokusanya katika mauzo ya korosho nje ya nchi.

Siku tano za mjadala wa Bajeti ya Serikali ya mwaka wa fedha 2018/19 zimekuwa tamu kwa upande mmoja na chungu kwa upande mwingine baada ya wabunge kumbana Waziri wa Fedha na Mpango, Dk Philip Mpango katika hoja kuu sita.

Zipo hoja kadhaa, zikiwamo tano zitakazomfanya waziri akune kichwa zaidi kuzipatia majibu kutokana na kujitokeza kwa wingi katika mjadala huo ambao unahitimisha kesho Jumatatu, ikiwamo ya Serikali kutotaka kurejesha asilimia 65 ya ushuru iliyokusanya katika mauzo ya korosho nje ya nchi.

Masuala mengine mazito yaliyoibuka katika Bajeti hiyo ya Sh32.5 trilioni ni harufu ya ufisadi katika mradi wa stempu za kielektroniki, Deni la Taifa, uanzishwaji wa akaunti ya pamoja ya Serikali, kusuasua miradi ya gesi na kuondolewa kwa Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) kwenye taulo za kike.

Ushuru wa korosho moto

Suala hilo ni miongoni mwa masuala yanayosubiri majibu ya waziri Mpango kwa kuwa limezungumzwa sana na wabunge wa mikoa ya Lindi na Mtwara wakiitaka Serikali kurejesha kwa wakulima asilimia 65 ya fedha zinazotokana na mauzo ya korosho nje ya nchi, ili kuendeleza zao hilo.

Mbunge wa Mbunge wa Nanyamba (CCM), Abdallah Chikota anasema kwa miaka mitatu uwekezaji uliofanyika miaka ya nyuma uliinua uzalishaji wa zao hilo kwa mara mbili lakini kinachomsikitisha hivi sasa ni mambo yanayoendelea hivi sasa kulenga kulidhoofisha.

“Matokeo yake ni kuwa ile sheria ya korosho ambayo inasema kuwa asilimia 35 ya Export Levy (Ushuru wa mauzo ya nje ya nchi) utakwenda mfuko mkuu wa Serikali inakwenda kufutwa na nimechungulia katika finance bill (Sheria ya Matumizi ya Fedha) ipo inafutwa ili pesa zote ziingie katika mfuko mkuu,” anasema.

“Hapa mnaua korosho. Hapa mnafanya siasa ya mikoa ya Lindi na Mtwara iwe ngumu. Na ndugu zangu waheshimiwa wabunge tuungane, kwa taarifa ya

Kituo cha Utafiti cha Naliendele hivi sasa wamejikita katika mikoa 17. Wale wenzangu wa Tabora wa Chunya fedha hii ikiondoka hamtawaona wataalamu,” anasema.

Mbunge wa Mtwara Mjini (CUF) Nachuma Maftaha anataka Serikali kutoa fedha hizo, Sh210 bilioni, kwa wakulima wa korosho katika mikoa ya kusini kwa kuwa sheria huwa hairudi nyuma.

“Wananchi wa mikoa ya Mtwara na Lindi ambao ndio wakulima wa korosho mwaka huu wamekosa Salfa. wanataka fedha ziletwe hata kama ni kwa mwaka ujao wa fedha la sivyo wataandamana,” anasema.

Maftaha anaungwa mkono na Mbunge wa Nachingwea (CCM), Hassan Masala kuwa mwaka 2015 wakati wanaingia bungeni kwa mara ya kwanza, walitoa mapendekezo ya jinsi ya kuboresha zao la korosho na mazao mbalimbali ili kuongeza tija kwa wakulima na Taifa kwa ujumla, hasa kuondoa tozo kadhaa.

“Nimepata mashaka juu ya mapendekezo ambayo Waziri Mpango ameleta, jambo hili kwetu sisi wakulima hamtakuwa mmetusaidia, na wazo hili ambalo Mpango umewaza kulileta, hebu fikiria kuliondoa kwani unataka kutugombanisha na wananchi,” anasema.

Mbunge mwingine aliyechangia hoja hiyo akiguzia maandamano ni wa Kilwa Kusini (CUF), Selemani Bungara maarufu kama Bwege anayesema endapo Serikali haitatoa asilimia 65 ya mauzo ya korosho nje ya nchi kwa wakulima wa mikoa ya Kusini hadi Juni 30, wakulima na wabunge wataandamana.

“Mheshimiwa Spika ikifika Juni 30 kama hela haijatoka uje (Ndugai) upokee maandamano yetu maana Serikali ya CCM inafanya kazi kama patasi ambayo haifanyi kazi mpaka igongwe. Wabunge wa Mkoa wa Lindi tutaandamana hadi asubuhi hadi mtoe fedha zetu,” anasema.

Kwa msisitizo, mbuge huyo anasema endapo Serikali haitatoa fedha hizo hadi kufikia muda huo ‘varangati’ kama lililokuwa wakati wa miradi ya gesi inaanzishwa litaanza upya katika mikoa hiyo.

“Wabunge wa mikoa ya kusini tuungane tupambane huyu Mpango (Dk Mpango) ana matatizo sana,” anasema.

Mbali na wabunge wa kusini, wabunge wengine waliochangia hoja hiyo ni pamoja na Abdallah Bulembo (Kuteuliwa-CCM) na Zitto Kabwe (Kigoma Mjini-ACT-Wazalendo).

Miradi ya gesi, mafuta

Kama ni mjadala kuwa ‘moto’, hali hiyo pia ilijionyesha wakati wabunge wanazungumzia suala la mafuta na gesi.

Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Bajeti, Hawa Ghasia na wanasema takwimu zinaonesha shughuli za utafutaji na uwekezaji wa mafuta na gesi zimekuwa zikipungua siku hadi siku na hivyo kushindwa kukidhi matarajio ya Serikali katika sekta hii kuweza kuchangia bajeti ya Serikali.

“Hivi karibuni tumeshuhudia kampuni kubwa ya kimarekani ya Exxon Mobil ikionyesha nia ya kuuza visima vyake vya gesi nchini ya kuwa ilianza mchakato wa kuwekeza kwa njia ya kuchangia mtaji katika mradi wa LNG Likongo mkoani Lindi,” anasema.

Anasema Serikali katika mapendekezo yake ambayo itapigiwa kura keshokutwa Jumanne haijaeleza mkakati wowote katika kuhakikisha inapata mapato yatokanayo na shughuli za utafutaji na uwekezaji wa mafuta na gesi nchini.

“Pia, taarifa ya hali ya uchumi wa Taifa kwa mwaka wa 2017 imeshindwa kuchambua hali ya maendeleo sekta ya mafuta na gesi,” anasema.

Ghasia aliishauri Serikali kufanya tafiti na kuona nini hasa kimechangia kupungua kwa shughuli za utafutaji mafuta na gesi na nini kifanyike kwa haraka kurekebisha kasoro hiyo na hivyo kuendelea kupata mapato kutoka katika sekta ya gesi.

Anasema sura ya bajeti inatakiwa ionyeshe kiasi cha mapato yaliyopatikana kwenye shughuli za utafutaji na uwekezaji wa mafuta na gesi.

Deni la Taifa

Kwa siku za karibuni, mjadala wa deni la taifa nao umekuwa mkubwa huku kukiwapo majibu yanayoendelea kuzua maswali.

Kuhusu suala hilo, Ghasia anashauri fedha zinazopatikana kutokana na mikopo zielekezwe kwenye miradi ya maendeleo ambayo itachochea ukuaji wa uchumi.

Anasema deni la Taifa la Sh10 trilioni bado linachukua asilimia 30 ya bajeti yote ya Serikali huku asilimia 49 ni matumizi ya kawaida.

“Changamoto iliyopo ni katika maeneo mawili tu (Deni la Taifa na mishahara) ambayo yamechukua Sh17.3 trilioni sawa na asilimia 53 ya bajeti yote. Huu sio uwiano mzuri hata kidogo kwa utekelezaji wa bajeti ya Serikali,” anasema.

Anasema ingawa deni hilo haliepukiki lakini ni mzigo mkubwa katika utekelezaji bajeti ya Serikali kwa kuwa linaathiri upatikanaji wa fedha za matumizi mengineyo (OC) kwa mafungu mbalimbali na kutaka jitihada zitumike katika kuhakikisha ulipaji unapungua.

VAT kwenye taulo za kike

Miongoni mwa mambo yaliyoshangiliwa wakati wa uwasilishaji bajeti ni kuondolewa VAT katika taulo za kike. Wabunge wengi wamepongeza hatua hiyo lakini wakiwa na angalizo kuwa punguzo hilo si la kutosha.

Kamati inasema hatua ya Serikali kusamehe kodi ya ongezeko la thamani (VAT) kwenye taulo za kike ili kuwezesha kupatikana kwa bei nafuu haitakuwa na manufaa kwenye mabadiliko bei.

“Kusamehe VAT kwenye taulo za kike kunawafanya wazalishaji wa ndani kushindwa kurejeshewa kodi hiyo waliyolipia katika malighafi walizotumia (Input tax claims),” anasema.

Anasema msamaha huo unawanufaisha zaidi wazalishaji wa nje wanaoleta bidhaa hiyo nchini kuliko wazalishaji wa ndani.

“Kamati inashauri Serikali kufanya marekebisho ya Sheria ya VAT sura 148 kifungu cha (6) ili kutoa fursa ya wazalishaji wa ndani kurejeshewa VAT watakazokuwa wamelipa wakati wa ununuzi wa malighafi (Input tax claims),” anasema.

Madaraka kwa halmashauri

Hoja nyingine ilikuwa ni kuzinyima halmashauri vyanzo vya mapato na fedha zote kupelekwa serikali kuu. Mbunge wa Tarime Vijijini (Chadema) John Heche anasema Dk Mpango atakuwa waziri wa kwanza kuua halmashauri zote nchini kwa kitendo chake cha kuchukua vyanzo vya mapato vyote na kupeleka Serikali Kuu.

“Fedha zote zinakusanywa na kuwekwa katika akaunti ya pamoja. Tuna vijiji 18,000 nchi nzima, kijiji kimoja kikiwa na shida ya hela unamwambia Mpango, hamtaweza, hii siyo Rwanda. Mnataka kuweka kila kitu Dodoma. Msitake kuua nchi hii,” anasema.

Heche anaiunga mkono Kamati ya Bunge ya Bajeti ambayo inasema ushuru wa mazao kuingizwa mfuko mkuu Kuhusu pendekezo la Serikali kuingiza makusanyo ya ushuru katika Mfuko Mkuu wa Serikali, itakuwa ni msumari wa mwisho kwenye jeneza la mazao ya biashara ya korosho, karafuu, katani, chai, tumbaku, pamba na kahawa.

“Kamati inashauri Serikali kuendelea kuziachia bodi zote za mazao fedha zinazokusanywa kutoka kwa wakulima kwa ajili ya uendelezaji wake na si vinginevyo,” anasema Ghasia.