Weusi majuu wana mawili; nidhamu au bangi na ulemavu wa akili

Muktasari:

  • Mosi video ya kijana mweusi aliyechomwa kisu shingoni ilisambazwa London, Uingereza. Alivamiwa na wenzake katika basi. Haya haya mabasi mekundu ya ghorofa.

Mambo matatu yalitokea mkumbo wakati Ufaransa iliponyakua Kombe la Dunia.

Mosi video ya kijana mweusi aliyechomwa kisu shingoni ilisambazwa London, Uingereza. Alivamiwa na wenzake katika basi. Haya haya mabasi mekundu ya ghorofa.

Vijana hupenda kupanda ghorofani ilhali wazee na watu wa makamo hupenda chini. Huko juu hutokea tafrani za kila aina. Kelele za muziki wa simu na uvutaji bangi. Kifupi video ilidhihirisha London na mji mkuu wa Uingereza unavyoendelea kuhatarika. Wiki hii idadi ya vifo vya mwaka 2018 imefikia 82. Huku nyuma runinga zilionyesha Ufaransa ikitwaa Kombe la Dunia.

Kijana Kylan Mbappe (19), mshambuliaji mwenye asili ya Afrika, kwa kuwa baba yake ni Mcameroon na mama mcheza netiboli wa Algeria akibeba kombe na kuishagilia Ufaransa ambapo bao lake lilimpa sifa ya pekee. Mbappe akalinganishwa na magwiji Thiery Henry, Ronaldo na mfalme Pele.

Kwa wasiomjua sawasawa Pele alikuwa na nguvu, mbio, chenga na mfungaji mzuri. Licha ya ugolikipa mwanariadha Pele aliruka viunzi, mbio fupi za kasi, kuogelea na mipira ya nyavu.

Mbappe anawaka. Sasa wakati sifa hizo zikiendelea, mitaani London omba omba hasa weusi wanaongezeka. Wapo wanaotukana ukiwanyima fedha za tumbaku. Wapo wenye ulemavu wa akili kutokana na kushindwa kumudu maisha. Ukichunguza bangi na dawa za kulevya zinachangia hayo.

Nilikuwa nikiongea na vijana fulani nilioshiriki nao kupiga muziki katika matamasha lukuki ya kiangazi yanayochemka jijini hapa hivi sasa.

Nikawauliza vipi mbona hawatumii dawa za kulevya? Maana chipukizi wengi hudhani ili kupiga muziki vizuri lazima ufanye ushetani huu. Mmoja akajibu, “kwa kijana London ni rahisi sana kupata widi au pombe. Kama si kuvuta au kunusa, unaombwa uuze. Hela rahisi sana. Vishawishi vingi. Unaona watu maarufu wakiendesha magari mazuri mazuri. Unawasikia watu wazima wakilalamika maisha ghali unaonyeshwa hela rahisi.Vigumu sana kukataa.”

Na maradhi ya akili ni moja ya matokeo ya dawa za kulevya. Ulemavu huu huenea mwilini.

Takwimu zinazotoka Afrika zinatueleza leo kuwa binadamu chini ya miaka 30 wanafariki dunia haraka kuliko zamani. Wanawake wanalalamika namna vijana wanavyotumia dawa ya viagra kufanya mapenzi. Viagra ilitengenezwa rasmi kwa wazee, lakini leo vijana wanatumia viagra.

Karibuni, London, tatizo la ulemavu wa akili limezidi hasa kwa watu weusi. Wapo wanaoilaumu Serikali ya Chama cha Conservative (Tories). Kwamba inawajali zaidi matajiri. Upo ukweli, lakini pia ukichunguza tatizo ni vijana wenyewe kukosa mwelekeo.

Kushindwa kwa timu ya Uingereza katika Kombe la Dunia kumewaumiza sana kisaikolojia baadhi ya vijana. Timu ya Waingereza ina vijana wenye nidhamu kama Harry Kane, nahodha aliyeshinda zawadi ya mfungaji mabao mengi.

Hata hivyo, baada ya Wafaransa kushinda wazo kuu moja limejizatiti. Takriban timu nzima ina Waafrika. Mbappe, Ng’olo Kante (Mali), Paul Pogba (Angola), Ousmane Dembele (Senegal na Mauritania), Blaise Matuidi (DRC /Angola) na kadhalika.

Ushindi kwao umeridhihirisha mtoto akilelewa vyema, akiwa na nidhamu anafaulu. Vijana hawa wana umri kati ya miaka 19 (Mbappe) hadi 33 (Matuidi).