Zilikuwa fainali za Mbappe na Modric

Muktasari:

  • Fainali hizo zilianza Juni 14 na kumalizika Julai 15 ambapo mabao 169 yalifungwa na kuweka rekodi katika historia ya fainali hizo.

Moscow, Russia. Fainali za Kombe la Dunia 2018 zimemalizika na Ufaransa imetwaa ubingwa baada ya kuifunga Croatia mabao 4-2 mjini Moscow, Russia.

Fainali hizo zilianza Juni 14 na kumalizika Julai 15 ambapo mabao 169 yalifungwa na kuweka rekodi katika historia ya fainali hizo.

Fainali hizo hazikuwa za kufurahisha kwa mastaa Lionel Messi wa Argentina na Cristiano Ronaldo wa Ureno ambao walishindwa kuzing’arisha timu zao. Fainali za mwaka huu zimekuwa na maajabu mbali na wachezaji nyota kushindwa kutamba, timu zilizokuwa zikipewa nafasi ya kutwaa ubingwa ziling’olewa mapema.

Mchezaji Bora

Nahodha wa Croatia Luka Modric alitwaa tuzo ya mchezaji bora wa fainali baada ya kucheza kwa kiwango bora na kuisaidia timu hiyo kufika fainali. Kiungo huyo alikuwa mhimili wa Croatia katika fainali hizo baada ya kutengeneza pacha maridadi na Ivan Rakitic.

Mchezaji Bora Chipukizi

Mshambualiaji chipukizi wa Ufaransa, Kylian Mbappe mwenye miaka 19, anayecheza Paris Saint-Germain (PSG) alitwaa tuzo ya mchezaji bora chipukizi.

Kinda huyo anatabiriwa kuchomoza katika tuzo ya Mchezaji Bora wa Mwaka ‘Ballon d’Or’.

Mfungaji Bora

Harry Kane, alitwaa tuzo ya mfungaji bora baada ya mabao sita kuifikisha nusu fainali England.

Kane anastahili kuwa mshambuliaji bora wa fainali kwa kuwa licha ya kubeba dhama kubwa ya unahodha kwa mara ya kwanza akiwa na miaka 24.

Kipa Bora

Thibaut Courtois wa Ubelgiji alitwaa tuzo ya kipa bora wa fainali hizo baada ya kulinda vyema lango.

Thibaut Courtois, aliiwezesha Ubelgiji kufika nusu fainali na kushika nafasi ya tatu katika fainali hizo. Kipa huyo wa Chelsea, amefungwa mabao sita katika mechi saba alizocheza kuanzia hatua ya makundi hadi nusu fainali.

Kocha Roberto Martinez anamtaja Courtois ni hazina ya Ubelgiji baada ya kumzima nyota wa Brazil Neymar katika mchezo wa obo fainali.

Timu Bora

Hispania ambao ni mabingwa wa Kombe la Dunia mwaka 2010, iliaga mapema katika fainali lakini hatua hiyo haikuwazuia kutwaa tuzo ya timu bora.

Hispania imechaguliwa timu bora yenye mchezo wa kiungwana ‘fair play’, baada ya wachezaji wake kucheza kwa nidhamu na kutopata kadi ya njano.