Makalla apokea vilio vya riba

Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Amos Makalla

Muktasari:

Kumekuwa na malalamiko ya kiwango cha riba kinachotozwa na wakopeshaji, lakini ya Mbeya ni ya kwanza

Mbeya. Mikopo ya riba kubwa inayotolewa na watu mbalimbali jijini hapa, ‘imewaliza’ watu wawili ambao walilazimika kuomba msaada kwa Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Amos Makalla aliposikiliza kero za wananchi kwenye Ukumbi wa Halmashauri ya Mbeya.

Makalla amejiwekea utaratibu wa kila Alhamisi ya mwanzo na mwisho wa mwezi, anasikiliza matatizo ya wananchi mbalimbali.

Jana, takriban watu 100 walifika wakiwa na kero akiwamo Magdalena Nyemba wa Mtaa wa Uyole, ambaye aliongozana na watoto wake; Maria na Violet Mwambene akidai analala nje baada ya nyumba yake kufungwa kwa makufuli makubwa.

Magdalena alisema alikopa Sh3 milioni za riba kwa mkopeshaji (jina limehifadhiwa) baada ya kukubali kurudisha Sh6 milioni kwa miezi mitatu.

“Kwa kweli nilimlipa Sh1 milioni mara ya kwanza, alinipeleka Baraza la Ardhi ambako niliagizwa nimlipe fedha zote au watauza nyumba yangu,” alisema.

Aliongeza kuwa juzi alifika mwanamke mmoja akiwa na lori kubwa nyumbani kwake, alisomba vitu vyote ikiwamo fedha na nguo za watoto kisha alifunga nyumba.

Mzee Angolile Kamenya wa Mtaa wa Forest ya Zamani, alimweleza Makalla kuwa familia yake imesambaratika baada ya nyumba yake kuuzwa kutokana na yeye na wenzake tisa kushindwa kurejesha Sh13 milioni.

Akifafanua kuwa yeye na wenzake tisa walikopa Sh10 milioni, kwa makubaliano ya kurejesha Sh13 milioni ndani ya mwezi mmoja.

“Baada ya mwezi kumalizika huku wenzangu wengine wakishindwa kurudisha deni, (anamtaja) ameikamata nyumba yangu na kuiuza akiniacha mimi na familia yangu nje,” alisema.

Kutokana na hoja hizo, Makalla alimuagiza Mkuu wa Kituo Kikuu cha Polisi, James Chacha kufuatilia taarifa za wanaokopesha fedha hizo na kutoza riba kubwa kama wanafuata sheria za nchi.

Katibu Tawala Mkoa, Mariam Mtunguja alisema watu wanaokopesha fedha kwa riba kubwa wanahatarisha maisha ya wananchi.

“Hakuna chombo cha fedha ambacho kinamkopesha mtu Sh3 milioni, kikataka faida ya Sh3 milioni ndani ya miezi mitatu,” alisema Mtunguja.