Makalla ashauri viongozi wa dini, mila watumike kupambana na ajali

Mkuu wa Mkoa Mbeya Amos Makalla, (Katikati) akizungumza na viongozi wa dini Askofu wa kanisa la Evangelical Brother hood Tanzania Robbi Mwakanani (kulia)  na  Imamu wa Msikiti Mkuu Shekhe Hassan Katanga wakati wa mkutano ulioshirikisha viongozi wa dini,wazee wa kimila  kujadili namna ya kukabiliana na matukio ya Imani za kishirikina. Picha na Hawa Mathias

Muktasari:

  • Makalla aliyasema hayo juzi wakati akizungumzia ajali iliyoua watu watano, iliyohusisha gari dogo aina ya Noah na lori, ikiwa ni siku chache baada ya ajali nyingine kuua watu zaidi ya 20.

Mbeya. Ajali za barabarani zilizofululiza mkoani Mbeya ndani ya kipindi kifupi, zimemfanya Mkuu wa Mkoa huo, Amos Makalla kushauri sasa watumike viongozi wa dini na wa kimila ili kuepusha hali hiyo.

Makalla aliyasema hayo juzi wakati akizungumzia ajali iliyoua watu watano, iliyohusisha gari dogo aina ya Noah na lori, ikiwa ni siku chache baada ya ajali nyingine kuua watu zaidi ya 20.

“Licha ya serikali mkoa kuendelea kutekeleza magizo yaliyotolewa na Waziri wa Mambo ya Ndani, Kangi Lugola juzi, kwa hali hii inatupasa kufikiria mbinu zaidi za kukabiliana na ajali, hii ni pamoja na kushirikisha viongozi wa dini na viongozi wa mila katika kumuomba Mungu atuepushe na ajali za aina hii,” alisema Makalla.

Ajali hiyo ya Julai 5 usiku pia imehusisha lori la mizigo lililofeli breki likiwa kwenye mteremko mkali wa Igawilo, katika barabara Kuu ya Tanzania–Malawi na kuparamia magari mengine matatu kabla ya kupinduka na kulalia gari dogo aina ya Noah na kusababisha vifo hivyo.

Kamanda wa Kikosi cha Usalama barabarani Mkoa wa Mbeya, Leopord Fungu alisema chanzo cha ajali hiyo ni lori lililokuwa linatokea Kasumulu mpakani mwa Tanzania na Malawi kwenda nchini Rwanda.

Alisema lori hilo lililokuwa limebeba zaidi ya tani 28 za sukari lilipofika kwenye mteremko huo, lilipoteza mwelekeo na kuanza kugonga magari mengine kabla ya kupinduka.

Kamanda Fungu alisema baadaye lori hilo liliangukia gari dogo aina ya Noah lililokuwa limebeba watu watatu na kusababisha wawili kati yao kupoteza maisha papo hapo.

“Pia dereva wa lori na msaidizi wake nao walipoteza maisha kwenye ajali hiyo na mtu mwingine waliyekuwa naye, hivyo kusababisha vifo vilivyotokea kwenye ajali hiyo kufikia vitano,” alisema Fungu.

Fungu wakati akisema hayo alikuwa ameshashushwa cheo kutoka Mrakibu wa Polisi (SP) hadi Naibu Mrakibu wa Polisi (ASP). Waziri wa Mambo ya Ndani, Kangi Lugola alitangaza kumshusha cheo juzi kutokana na ongezeko la ajali mkoani humo.

Makalla alisema ajali ambazo zimetokea mfululizo mkoani Mbeya zinaliingizia taifa hasara kwa kupoteza mali na rasilimali watu hivyo ipo haja ya kubuni mbinu zaidi za kukabiliana na ajali hizo.

Ajali ya Julai 5, ni mfululizo wa ajali zinazotokea mkoani humo zikihusisha lori kulalia magari madogo ambapo Julai 2 mwaka huu, lori liliangukia mabasi madogo matatu na kusababisha vifo vya watu 20.

Juni 14, watu 13, walifariki dunia, wakiwamo vijana 11 waliokuwa mafunzoni wa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) katika mteremko wa Igodima, Mbeya.