Makamba ajitosa mradi wa umeme wa Stiegler’s Gorge

Muktasari:

Amezungumzia mradi huo wakati akihojiwa na Redio Clouds 

Dar es Salaam. Saa 24 baada ya mradi wa umeme wa Stiegler’s Gorge katika Pori la Akiba la Hifadhi ya Selous kutikisa Bunge, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu Rais (Muungano na Mazingira), January Makamba amewataka Watanzania kutulia na kubainisha kuwa tathmini ya mradi huo inafanyika.

Makamba ametoa kauli hiyo leo Jumatano Mei 23, 2018 wakati akihojiwa katika kipindi cha Power Breakfast kinachorushwa na Redio Clouds.

Jana bungeni mjini Dodoma mradi huo ulikuwa gumzo wakati wabunge wakijadili bajeti ya Wizara ya Maliasili na Utalii ya mwaka wa fedha 2018/19, ambapo baadhi ya wawakilishi hao wa wananchi akiwemo Nape Nnauye (Mtama) na Zitto Kabwe (Kigoma Mjini), walitaka tathmini ifanyike kabla ya kuanza kwa mradi huo.

Wamehoji kitendo cha Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) kutangaza tenda ya kukata miti katika pori hilo, tenda inayohusisha ukataji miti zaidi ya mita za ujazo 3,495 na kwamba idadi ya miti inayokatwa ni sawa na ukubwa wa Mkoa wa Dar es Salaam huku ikijulikana  wazi kuwa tathmini bado haijakamilika.

 

 

Katika maelezo yake ya leo, Makamba amesema  tathmini inafanyika ili kujua athari  na namna ya kukabiliana nazo, “lazima sheria ifuatwe ikiwamo kufanya tathmini ya athari ya mazingira, ndicho kinachofanyika hivi sasa kuhusu mradi huo.”

“Tanesco walikuja NEMC (Baraza la Taifa la Uhifadhi na Usimamizi wa Mazingira)  kusajili mradi wa Stigle’s Gorge ili kufanya tathmini ya mazingira. Baada ya kuandikisha Tanesco walimchagua mshauri ambaye ni Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kwa sababu ni kazi ya kisayansi.”

Makamba amesema tayari shirika hilo limeshapeleka ripoti katika ofisi yake baada ya kufanya tathmini hiyo na kinachofuata ni NEMC  kutuma timu kwa ajili ya kujiridhisha kuhusu yaliyoandikwa katika mradi na yanayoonekana kama ni kweli.

Amesema baada ya hapo kamati ya ufundi ya ushauri itazungumza  na wadau wote katika eneo la mradi na kuthibitisha taarifa zilizopo kuhusu mradi husika.