Makamba ataja madudu yaliyobainika ukamatwaji wa viroba

Muktasari:

Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake jana, Waziri Makamba alisema jumla ya katoni 99,171 za viroba zilikamatwa katika operesheni iliyofanyika kwa siku tatu mfululizo nchi nzima.

Dar es Salaam. Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), January Makamba, amesema kampuni zote zilizokamatwa zikitengeneza pombe za viroba hazina vyeti vya Tathmini ya Athari kwa Mazingira (EIA) na nyingine hazijalipa kodi ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na pia hazina cheti cha Shirika la Viwango Tanzania  (TBS).

Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake jana, Waziri Makamba alisema jumla ya katoni 99,171 za viroba zilikamatwa katika operesheni iliyofanyika kwa siku tatu mfululizo nchi nzima.

“Na pombe nyingi zilizopo kwenye viroba zinafungwa kwenye karatasi ambazo zimeshatumika,” alisema Makamba.

Alisema kikosi hicho pia kiligundua kwamba kuna kampuni nyingi zilikuwa zikisafirisha mizigo ya viroba usiku wa manane wakati ukaguzi ukiendelea.

Alisema viroba vyenye thamani ya Sh235 milioni vilikutwa kwenye maghala ya maduka ya jumla chini ya jengo moja la ghorofa ambalo lipo kama handaki eneo la Kariakoo jijini Dar es Salaam.

Waziri Makamba alisema kwenye ukaguzi huo pia ilibainika pombe kali aina mbalimbali zilizofungashwa katika viroba na chupa hazikuwa na namba ya matoleo (batch numbers) na tarehe za uzalishaji kwenye lebo.

Habari zaidi soma Gazeti la Mwananchi