Monday, March 20, 2017

Makamba awapa siku 30 wakazi kuvunja nyumba

 

By Bakari Kiango, Mwananchi bkiango@mwananchi.co.tz

Bagamoyo. Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), January Makamba amewapa mwezi mmoja wakazi wa Mpigi Darajani Kata ya Mapinga wilayani hapa kuvunja nyumba zilizojengwa kinyume cha sheria kando kando ya Mto Mpigi.

Makambq alitoa kauli hiyo leo (Jumatatu) alipotembelea eneo hili kujionea shughuli za mazingira na uhabifu wake katika wilaya ya Bagamoyo mkoa wa Pwani.

Awali Makamba ambaye Mbunge wa Bumbuli Tanga alitoa wiki mbili nyumba hizo zibomolewe lakini balozi wa eneo Julius Mapunda alimuomba kupewa muda zaidi ili wajipange.

Makamba amesema nyumba hizo zitabomolewa kwa gharama za wakazi hao kwa kuwa wamevunja kanuni na taratibu kwa mujibu wa Sheria ya Mazingira ya 2004.

Pia alitumia nafasi kumwagiza Mapunda kupiga marufuku watu kulima tena katika maeneo hayo ya kando kando ya mto ili kuhifadhi mazingira.

Mapunda amesema eneo hilo lina nyumba zaidi ya 200 na kuna baadhi zilivunjwa awamu ya kwanza, hivi sasa bado hajui ni ngapi zitabomolewa.

-->