Makamba kukarabati jengo la wakoloni liwe hosteli

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), January Makamba.

Bumbuli. Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), January Makamba amesema  wanampango wa kukarabati jengo lilokuwa linatumiwa na Wakoloni na ambalo lilitaifishwa na Serikali wakati wa Azimio la Arusha mwaka 1967 ili litumike kama hosteli ya wasichana Bumbuli.

Makamba ambaye pia ni mbunge wa Bumbuli amesema hayo leo alipofika kukagua jengo hilo lilopo Shule ya Sekondari ya Baga, ambapo alisema ukarabati huo wa jengo hilo utakapo kamilika  litakuwa na uwezo wakuchukua wanafunzi wakike zaidi ya 100.

"Tutatuma mkandarasi ili aje afanye tathimini ili kujua gharama za ukarabati wa jengo hilo," amesema Makamba.

Makamba amesema kuwa wanafunzi wa kike wengi wanakumbana na vishawishi vingi wanapokuwa mtaani hivyo hostel hiyo itasaidia kwa kiasi kikubwa kuondokana na vishawishi hivyo.

Makamba yuko kwenye ziara ya siku tano yenye lengo la kukagua utekelezaji wa miradi ya maendeleo na utekelezaji wa ilani ya CCM.