Majaliwa akagua makazi ya Makamu wa Rais

Muktasari:

Mhagama amesema kazi ya matengenezo itagharimu Sh1.5 bilioni.

Dar es Salaam. Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amekagua matengenezo ya makazi ya muda yanayotarajiwa kutumiwa na Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan atakapohamia Dodoma.

Waziri mkuu amefanya ukaguzi huo leo Jumatano, Desemba 6, 2017 mchana  katika eneo la Kilimani mjini Dodoma ambako yalikuwa makazi ya mkuu wa mkoa.

Akitoa taarifa ya ujenzi, Waziri wa Sera, Uratibu, Bunge, Kazi, Ajira, Wenye Ulemavu na Vijana, Jenista Mhagama amesema kikosi kazi cha kuratibu kazi ya Serikali kuhamia Dodoma kilibaini mahali alipokuwa akiishi awali si sahihi kwa ajili ya makazi ya kudumu ya Makamu wa Rais.

“Pale palikuwa panafaa kwa ajili ya ziara za kikazi alipokuwa akija Dodoma, kwa hiyo tumeamua tufanye ukarabati hapa ili aweze kuishi kwa viwango vinavyostahili,” amesema katika taarifa iliyotolewa na Ofisi ya Waziri Mkuu.

Amesema kazi ya matengenezo itagharimu Sh1.5 bilioni wakati kazi ya kutenganisha ofisi za watumishi na wasaidizi wa Makamu wa Rais itagharimu Sh680 milioni.

Waziri mkuu pia amekagua matengenezo ya ofisi inayotarajiwa kutumiwa na Makamu wa Rais ambayo itakuwa eneo la Ndejengwa.

Kaimu Meneja wa Wakala wa Majengo (TBA) Mkoa wa Dodoma, Steven Simba anayesimamia ujenzi huo amesema wanataraji kazi itakamilika kabla ya Desemba 30,2017.