Makamu wa Rais awataka wapelelezi, waendesha mashtaka waepuke rushwa

Muktasari:

Mama Samia ametoa kauli hiyo leo (Jumatano) wakati akizindua mwongozo kwa wapelelezi na waendesha mashtaka wa kesi za wanyamapori na misitu katika Ukumbi wa Kimataifa wa Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam.

 Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan amewaagiza wapelelezi na waendesha mashtaka nchini waepuke vitendo vya rushwa na badala yake wafanye kazi kwa bidii kwa kuweka maslahi ya taifa mbele.

Mama Samia ametoa kauli hiyo leo (Jumatano) wakati akizindua mwongozo kwa wapelelezi na waendesha mashtaka wa kesi za wanyamapori na misitu katika Ukumbi wa Kimataifa wa Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam.

Amesema mwongozo aliouzindua utasaidia kwa kiwango kikubwa uboreshwaji wa upelelezi na uendeshaji wa kesi zinazohusu wanyamapori na misitu nchini.

“Uwepo wa mwongozo huu ni dhahiri unategemewa kutoa matokeo chanya katika mapambano dhidi ya ujangili na uhalifu katika misitu yetu,” amesisitiza

Amesema kuwa ana imani mwongozo aliouzindua utasaidia kukomesha vitendo vya uhalifu ambavyo vimekuwa vikiisababishia Serikali hasara kubwa ikiwamo uharibifu wa rasilimali za Taifa na kupoteza mapato ambayo yangesaidia kuimarisha huduma za kijamii nchini.

Kuhusu sekta ya utalii nchini, Makamu wa Rais amesema pamoja na sekta hiyo kuliingizia taifa mapato mazuri lakini inasikitisha kuona kuwa uwepo wa wanyamapori ambao ndio nguzo kuu ya sekta ya utalii ukipungua kila kukicha na hivyo kuwa tishio kubwa kwa uchumi na nchi.

Amesema vitendo vya ujangili vimeendelea kuangamiza wanyama hasa tembo hivyo ni muhimu kwa wapelelezi na waendesha mashtaka kutenda haki bila kuonea mtu.

“Wazee wetu walilinda na kutunza rasilimali zetu kwa faida yetu, nasi tuzitunze kwa ajili ya vizazi vijavyo,” ameeleza Makamu wa Rais.

Kwa upande wake, Waziri wa Maliasili na Utalii, Profesa Jumanne Maghembe amemhakikishia Makamu wa Rais kuwa kazi ya kupambana na ujangili na utoroshaji holela wa wanyama na viumbe wengine itakuwa endelevu na watakaokamatwa watachukuliwa hatua kali za kisheria ili kukomesha vitendo hivyo.

Profesa Maghembe amemwomba Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini kuendesha operesheni maalum ya kukusanya silaha zote ambazo zimekuwa zikitumika kwenye ujangili ili kuhakikisha wanyama hasa tembo wanakuwa salama kwenye maeneo ya Hifadhi za Taifa nchini.

Kwa upande wake, Mwendesha Mashtaka Mkuu wa Serikali, Biswalo Mganga amefafanua kuwa katika kipindi cha mwaka 2014 na 2017 ofisi yake imewafikisha mahakamani washtakiwa wakubwa wa ujangili ambao walikuhumiwa vifungo virefu na faini.

Amesema kuwa washtakiwa 100 walihukumiwa kulipa faini ya zaidi ya shilingi bilioni 1.1 kwa kujihusisha na nyara za Serikali kinyume na sheria na faini hizo zimeshalipwa.

Ameeleza kuwa kati ya idadi hiyo watuhumiwa zaidi ya 80 walihukumiwa kifungo cha miaka 20 hadi 30 gerezani na faini ya zaidi ya Sh164 milioni ambazo bado hazijalipwa.

Mganga amesema kuwa mafanikio hayo yote yamechangiwa na usimamizi madhubuti wa kesi hizo kupitia dawati la wanyamapori katika Divisheni ya Mashtaka pamoja na Mawakili wa Serikali katika ofisi zote za mikoani nchini.