Makamu wa Rais wa Cuba kutua nchini kesho

Muktasari:

Waziri wa Mambo ya Nje, Balozi Augustine Mahiga amesema lengo la ziara hiyo ni kuimarisha uhusiano baina ya Tanzania na Cuba ambao umedumu kwa zaidi ya miaka 50.

Dar es Salaam. Makamu wa Rais wa Cuba, Salvador Antonio Valdes Mesa anatarajiwa kuwasili nchini Oktoba 2, mwaka huu kwa ziara rasmi ya siku tatu.

Waziri wa Mambo ya Nje, Balozi Augustine Mahiga amesema lengo la ziara hiyo ni kuimarisha uhusiano baina ya Tanzania na Cuba ambao umedumu kwa zaidi ya miaka 50.

Amesema kiongozi huyo atapokelewa na Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan na atafanya mazungumzo na Rais John Magufuli kabla ya kwenda zanzibar. Dk Mahiga amesisitiza kwamba Serikali imepanga kuongeza uhusiano na Cuba katika sekta za uwekezaji, kilimo hasa cha miwa na viwanda.

Mbali na ziara hiyo, Dk Mahiga amesema ziara yake katika Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa (UN) ilikuwa na mafanikio kwa sababu alipata kuzungumza na viongozi mbalimbali akiwemo Katibu Mkuu wa UN, Ban Ki Moon. Amesema alipata nafasi ya kueleza maafa ya Kagera na kwamba mataifa mbalimbali yameonyesha nia ya kuwachangia waathirika wa maafa hayo.