Makandarasi walalamika kutengwa miradi ya ujenzi nchini

Muktasari:

Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Usafirishaji),Dk Leonard Chamuriho alisema hayo jana jijini hapa wakati wa ufunguzi wa mkutano wa wahandisi washauri nchini ikiwa ni sehemu ya kuadhimisha miaka 50 ya kuanzishwa kwa Bodi ya Usajili wa Wahandisi (ERB) ambayo kilele chake ni Septemba.

Dar es Salaam. Wakati kampuni za ndani za makandarasi zikilalamikia kutengwa katika upatikanaji wa miradi ya ujenzi nchini, Serikali imesema changamoto hiyo inatokana na ushiriki mdogo wa kampuni hizo kwenye mikutano ya kuandaa kanuni zinazozingatia vigezo vya ushindani wa kupata kazi ya miradi ya ujenzi.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Usafirishaji),Dk Leonard Chamuriho alisema hayo jana jijini hapa wakati wa ufunguzi wa mkutano wa wahandisi washauri nchini ikiwa ni sehemu ya kuadhimisha miaka 50 ya kuanzishwa kwa Bodi ya Usajili wa Wahandisi (ERB) ambayo kilele chake ni Septemba.

Alisema kabla ya upatikanaji wa kazi, hufanyika tathmini ya kampuni husika kwa kuzingatia kanuni walizojiwekea akitolea mfano wa mradi mkubwa kutolewa kwa kigezo cha jumla ya thamani ya kazi zilizofanywa jambo ambalo kampuni za ndani zimeonekana kuwa chini ikilinganishwa na za kigeni.

“Kwa mfano ili upewe kazi, unakuta kuna kigezo cha kuangalia jumla ya thamani ya kazi za mkandarasi au mhandisi husika kwa mwaka, kwa hiyo mradi ukiwa mkubwa, kigezo hicho ni tatizo (kwa wazawa),” alisema Dk Chamuriho.

Hata hivyo, licha ya kigezo cha jumla ya thamani kuweza kuwa tatizo, alisema hakina uhusiano na uwezo mdogo wa kampuni kufanya kazi.

“Kama kazi (inayoshindaniwa) inajirudiarudia. Kwa mfano, unajenga nyumba ya Sh100 milioni, mradi unaotangazwa ni kujenga nyumba 1,000 za aina hiyohiyo, kwa hiyo thamani ya mradi itakuwa (kubwa) na kampuni za ndani zinaonekana haziwezi kumbe ni kazi ndogo iliyojirudiarudia ndiyo maana nawashauri wawe wanashiriki kuandaa kanuni,” alisema Dk Chamuriho.

Aliwataka wadau wote nchini wakiwamo makandarasi na wahandisi washauri kuhakikisha wanashiriki kwa wingi kwenye mikutano ya uandaaji wa kanuni hizo zinazoathiri masilahi yao kupitia mikutano ya Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA).

Dk Chamuriho alisema baadhi ya wadau ambao hutakiwa kushiriki katika uandaaji wa kanuni hizo chini ya PPRA ni pamoja na makandarasi na wahandisi washauri. Wadau wengine ni Wizara ya Ujenzi, Bodi ya Wahandisi Washauri na ERB.

Mwenyekiti wa ERB, Profesa Ninatubu Lema alisema changamoto iliyopo ni makandarasi na wahandisi wengi kubanwa na kazi nyingi hatua inayowakwamisha kushiriki katika mikutano ya kuandaa kanuni hizo.

“Wanakuwa very busy, wakiitwa wadau njooni tushiriki kutayarisha kanuni. Kwa hiyo Serikali inahamasisha kushiriki katika fursa ya kuandaa kanuni kwenye mikutano hiyo ili kutetea masilahi yao,” alisema Profesa Lema.

Kaimu Msajili wa Bodi ya Wahandisi Washauri, Patrick Barozi alisema mkutano utajadili na kupitisha mabadiliko ya vigezo vya utoaji wa kazi kwa wahandisi kwa kuzingatia vipaumbele vipya.

Mabadiliko yalipendekezwa na Lucas Choko yakilenga kuzitenga kampuni katika madaraja mbalimbali yanayoendana na aina ya miradi itakayokuwa ikishindaniwa.

“Katika mabadiliko hayo ya “Classification of engineering consulting firm”, yataweka kigezo cha thamani ya kazi zinazofanywa na kampuni, uzoefu wa kampuni, kiwango na ubora wa mainjinia wa kampuni, mabadiliko hayo hayataathiriwa na kanuni zinazoandaliwa na mikutano ya wadau chini ya PPRA,” alisema.

Mmoja Kati washiriki wa mkutano huo, Celestine Kazoba alisema licha ya kiwango kidogo cha ushiriki wa kuandaa kanuni hizo, ushindani na tathmini ambazo zimekuwa zikifanyika
hazisaidii kampuni za ndani. Alisema ERB imekuwa haitoi jukwaa la kujadili dosari za upatikanaji wa kazi za ndani.

Alisema Botswana imesaidia uandaaji wa kanuni zinazotoa vipaumbele kwa kampuni za ndani kuhakikisha zinapata kazi zenye viwango maalumu vilivyowekwa bila kujali ushindani uliopo kutoka kampuni za kigeni.