Makerere wahakiki shahada walizotoa

Muktasari:

  • Uhakiki wa alama walizopewa wanafunzi miaka 10 iliyopita unafanyika ambao utawezesha kufuta shahada za waliotunukiwa baada ya matokeo kughushiwa au kubadilishwa.

Chuo Kikuu cha Makerere kimeanza kufanya uhakiki wa kina wa alama walizokuwa wakipewa wanafunzi kuanzia miaka 10 iliyopita ili kubaini na kufuta shahada za waliotunukiwa baada ya matokeo kughushiwa au kubadilishwa.

Uchunguzi wa gazeti la The Monitor unaonyesha anayesimamia uhakiki huo ni Dk Damalie Naggitta-Musoke, mkuu wa zamani wa Shule ya Sheria.

Kazi ya uhakiki wa vyeti ilianza Novemba mwaka jana.

Tofauti zilizojitokeza kati ya matokeo yaliyowasilishwa na vyuo na shule ikilinganishwa na matokeo ya mwisho yaliyotolewa na Ofisi ya Taaluma zilichangia chuo kikuu kuongeza kipindi cha kuchunguza kufika miaka mitano.

Lakini habari kutoka ndani zinasema, katika shule ya sheria matokeo yanayopitiwa upya ni ya hadi muongo mmoja uliopita.

 

Wanaonyang’anywa

Vyanzo vya habari vinasema miongoni mwa watu wanaotarajiwa kuathiriwa na mchakato wa uhakiki wa vyeti kwa kuangalia uhalisia wa alama ni waziri wa zamani aliyetunukiwa shahada katika Utawala wa Umma.

Wengine ni wabunge kadhaa maarufu pamoja na wataalamu mashuhuri ambao hulipwa kwa kutoa ushauri. Majina ya watu mbalimbali ambao wataathiriwa yamehifadhiwa.