Makonda, Nape ni jino kwa jino

Dar es Salaam. Kauli ya mbunge wa Mtama, Nape Nnauye kuhusu kuongezeka kwa wimbi la wabunge na madiwani wanaohama vyama vyao na hivyo kulazimika kufanyika kwa chaguzi ndogo, limemuingiza katika vita ya maneno na mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda.

Nape alikakaririwa na vyombo vya habari juzi akisema, “Ifike mahali turuhusu mtu akihama chama, ahame na ubunge wake au cheo chake alichonacho.”

Lakini jana, Makonda akizungumza na Mwananchi alisema kauli za Nape zinaonyesha ana hofu ya mabadiliko ndani ya chama kwa kuwa yanafifisha nafasi yake (Nape) ya kupata fursa nyingine, kauli ambayo ilijibiwa na Nape alipotafutwa kutoa maoni yake akisema yeye ni mwanaCCM si kwa sababu ya vyeo au uteuzi bali kwa imani na itikadi.

Makonda alisema ameguswa na kauli na maandiko ya Nape kwa kuwa mkoa wake una jimbo na kata zitakazofanya uchaguzi wa marudio.

Agosti 16, Nape akifungua mafunzo ya siku mbili ya kamati ya uongozi, makamu wenyeviti wa kamati za Bunge na wajumbe wa Tume ya Utumishi wa Bunge, alisema ifike mahali turuhusu mtu akihama chama, ahame na ubunge wake au cheo alichonacho.

“Hii kitu ina ukakasi, ingawa haivunji sheria na kama ina ukakasi ni vizuri tukatengeneza forum (jukwaa) kwa ajili kusimamia sheria za mchezo huo katika mfumo wa vyama vingi,” alisema Nape.

Makonda alisema Mkoa wa Dar es Salaam, una uchaguzi wa Jimbo la Ukonga na kata mbalimbali na kwamba kauli hizo za Nape huenda zikafanya uchaguzi huo kuwa mgumu kwa sababu waliohama vyama wametumia haki yao ya msingi.

“Watu wanahama vyama baada ya kuona katiba, uongozi na ilani walikokuwa havifuatwi sasa kwa nini waendelee kukaa huko?” alisema Makonda ambaye alishawahi kuwa kiongozi wa UVCCM.

“Nimeamua kueleza haya baada ya kuona kauli na maandiko ya Nape katika mitandao ya kijamii na vyombo vya habari ikiwamo magazeti zikijirudia. Leo (jana) baadhi ya vyombo vya habari vimenukuu kauli ya Nape.”

Kuhusu hilo Nape alimjibu Makonda akisema, “Huyu ni mdogo wangu, namheshimu na kumtakia mema, ushauri wangu kwake ni kuwa ule ulikuwa ni uchambuzi wa kisomi, sayansi ya siasa. Kama shule ni ya kubangaiza huwezi kuelewa, hivyo kwa hili namsamehe.”

Nape alisema hivi karibuni Katibu Mkuu wa CCM, Dk Bashiru Ally alitoa taarifa inayoonyesha mikoa inayofanya vibaya kwenye uhusiano kati ya chama na Serikali na Dar es Salaam ilikuwa mmojawapo, “Nadhani angehangaika na hili kwanza, badala ya kuhangaika na hoja ambazo ziko juu ya uwezo wake.”

Katika hoja zake, Makonda alisema bado hajaelewa kinachomhangaisha Nape dhidi ya watu wanaojiunga na CCM baada ya kuridhishwa na utendaji kazi wa Rais John Magufuli.

“Kazi ya uitikadi na uenezi ni kushawishi watu wajiunge na chama chako na sidhani kama kuna mwanaCCM makini atakayejisikia vibaya kuongezeka kwa wanachama wapya. Huwezi kuona watu wanajiunga na chama chako halafu unaanza kunung’unika, maana kutakuwa na tatizo mahali.

“Nimejaribu kumpigia simu na kumtumia ujumbe mfupi kaka yangu (Nape), ili anifafanulie kuhusu kauli zake lakini hajibu nadhani hana namba zangu ila nitaendelea kumtafuta.”

Makonda alisema anachokiona kwa Nape ni hofu ya mabadiliko ndani ya CCM kutokana na ujio wa vijana wengi wenye uwezo ambao watahakikisha gurudumu la chama hicho tawala linasonga mbele. Alisema hofu hiyo inatokana na baadhi ya watu wenye udhaifu ndani CCM ambao wanahisi nafasi zao zitachukuliwa baada ya ingizo la vijana wanaohamia chama hicho tawala.

Makonda ambaye alisema anazungumza kama kada na mwanaCCM wa kawaida alisema, “Watu na hofu ndani ya CCM hawana uhakika na nafasi zao, hebu fikiria ndani ya chama tawala una mtu kama (Mwita)Waitara, David Kafulila, Albert Msando na Moses Machali ambao ni vijana makini.”

Kuhusu hoja ya ukakasi, Makonda alimshangaa Nape, “Kwa nini asipate ukakasi wakati wa kwenda kuwanadi kwenye kampeni watu hawa wanaohamia CCM?”

Makonda alisema katika miaka ya nyuma, Nape alikuwa mstari wa mbele kuwakosoa wapinzani akisema hawana demokrasia ya kweli katika vyama vyao.

“Hivi sasa anawashangaa watu wanaohama upinzani na kujiunga na CCM wakati huko nyuma yeye alikuwa akiukosoa upinzani huuhuu. Namshangaa kwa kauli zake…Mbona alipotoka Nyalandu sikumsikia akitoa kauli kama hizi? Sielewi kinamchomsumbua ni kitu gani wakati CCM inapata watu.”

Alisema mtu mpya akija ndani ya CCM apokewe na sio kuhoji na kwamba chama hicho kinasimamia demokrasia ya kuwapelekea wananchi wagombea walewale ili waamue.

“CCM haiwachagulii wananchi mgombea bali, ndio wenye uamuzi wa mwisho kumtaka mwakilishi kupitia sanduku la kura. Ndio maana maeneo yote wamerudishwa wagombea walewale,” alisema.

Alisema anatamani kuwaona wanasiasa wa Dar es Salaam, wakifikiria namna ya kuwaletea wananchi maendeleo na siyo kuimarisha upinzani.

“Narudia huu si wakati wa kuimarisha upinzani kwa mkoa huu, ni wakati wa kuijenga Tanzania. Wale waliochoshwa kwenye vyama vyao, wasipoteze muda waje tu CCM.”