Makonda ataka wahalifu wagongwe, wapigwe

Mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda

Muktasari:

Akizungumza wakati wa kuaga miili ya askari watatu kati ya wanne wa Jeshi la Polisi waliouawa wiki hii katika  tawi la benki ya CRDB lililopo Mbande wilayani Temeke jijini Dar es Salaam, Makonda alisema jambazi atakapokutwa popote iwe msituni iwe wapi agongwe na apigwe.

Dar es Salaam. Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda ameliagiza Jeshi la Polisi kuwagonga na kuwapiga wahalifu wowote wakiwamo majambazi pindi wanapowakamata.

Akizungumza wakati wa kuaga miili ya askari watatu kati ya wanne wa Jeshi la Polisi waliouawa wiki hii katika  tawi la benki ya CRDB lililopo Mbande wilayani Temeke jijini Dar es Salaam, Makonda alisema jambazi atakapokutwa popote iwe msituni iwe wapi agongwe na apigwe.

Alisema alipopata taarifa ya vifo vya askari hao wanne alifungua pazia za madirisha nyumbani kwake na kuwaangalia askari wanaolinda na kulia kwa uchungu na kwamba, usiendelezwe ukichaa wa haki za binadamu kwani ni uendawazimu ambao hauwezi kuvumilika.

“Kamanda Sirro (Simon) mimi ndiyo mkuu wako wa mkoa nasema ukikamata hao watu popote gonga, piga na watu wa haki za binadamu wakija waambie waje kwangu, hatuwezi kukaa kwenye mkoa ambao haupo salama,” alisema Makonda aliyedai hana maneno mazuri ya kusema kwa sababu hakuumbwa kumfurahisha mtu, bali anafanya kazi ya Mungu na wakati wake ukiisha ataondoka.

Habari zaidi soma Gazeti la Mwananchi