Makonda aungwa mkono vita dhidi ya dawa za kulevya

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda.

Muktasari:

  • Akizungumza na waandishi wa habari jana, Mwenyekiti wa Ojadact, Edwin Soko alisema hatua hiyo inapaswa kuungwa mkono na watu wengine.

Mwanza. Chama cha waandishi wa habari wa kupiga vita uhalifu na matumizi ya dawa za kulevya Tanzania (Ojadact), kimeunga mkono kazi ya kupiga vita dawa hizo iliyoanzishwa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda.

Akizungumza na waandishi wa habari jana, Mwenyekiti wa Ojadact, Edwin Soko alisema hatua hiyo inapaswa kuungwa mkono na watu wengine.

 “Kitendo cha kuwataja hadharani watu wanaodaiwa kujihusisha na mihadarati siyo jambo rahisi, lakini Makonda amethubutu asiachwe peke yake aungwe mkono,” alisema.

Hivi karibuni, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mwigulu Nchemba alisema tatizo la dawa za kulevya nchini limeongezeka kwa asilimia 6.5 mwaka 2015 ikilinganishwa na mwaka 2010 na watuhumiwa 247 wanashikiliwa na polisi kwa kujihusisha na biashara hiyo.