Makonda awaita polisi Wema, TID, Chid Benz

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda

Muktasari:

Miongoni mwa wa wasanii wanaotarajiwa kukutana na Makonda ni Khalid Mohamed (TID), Rashid Makwiro (Chid Benz), Wema Sepetu na Winfrida Josephat maarufu kama Recho.

Dar es Salaam. Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda leo atakutana na wasanii maarufu katika Kituo Kikuu cha Polisi, jijini hapa kuzungumzia juu ya kutajwatajwa kwao na matumizi ya dawa za kulevya.

Miongoni mwa wa wasanii wanaotarajiwa kukutana na Makonda ni Khalid Mohamed (TID), Rashid Makwiro (Chid Benz), Wema Sepetu na Winfrida Josephat maarufu kama Recho.

Mbali ya hao, Makonda alisema katika jitihada za kupambana na matumizi ya mihadarati, watu kadhaa wamekamatwa na wanahojiwa. Aliwataja watu hao kuwa ni Ahmed Ngahemela (Petit Man), Said Masoud Lina (Alteza), Nassor Mohamed Nassor, Bakari Mohamed Khelef na mwingine aliyemtaja kwa jina moja la Omary.

Akizungumza jana ofisini kwake, Makonda alisema anataka suala la dawa za kulevya liwe historia katika Mkoa wa Dar es Salaam na kwamba ametoa siku saba kutokomea kwa vijiwe vinavyojihusisha na ulevi huo.

“Nimeamua mwenyewe kuingia kwenye vita hii, niko tayari kupoteza ukuu wangu wa mkoa, niko tayari kupoteza maisha yangu ilimradi niwe na chakujibu nikifika mbinguni. Sitaki nikiulizwa na Mungu nilifanya nini kuhusu dawa ya kulevya nikose cha kujibu,” alisema.

Mbali na wasanii hao, Makonda aliwataja askari polisi tisa kwa madai kwamba wanajihusisha na biashara ya dawa za kulevya na kushirikiana na watumiaji. Katika orodha hiyo alimtaja pia aliyekuwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Christopher Fuime.

Alipulizwa kwa simu jana Fuime alisema, “Mkuu wa Mkoa amesema hizo ni tuhuma tu na mimi siwezi kufanyia kazi tuhuma mpaka itakapothibitishwa.”

“Kama Kamishna (Simon) Sirro na timu yake wameshindwa kutokomeza dawa za kulevya ndani ya Mkoa wa Dar es Salaam, basi maana yake wamekosa sifa na vigezo vya kuwa askari ndani ya mkoa huu,” alisema Makonda.

“Operesheni hii nafanya mwenyewe; situmi mtu, naenda mwenyewe. Ndiyo maana leo (jana) nimekesha kuhakikisha napata kila kitu kinachostahili kwa ajili ya mustakabali ya Taifa letu sambamba na kiapo ambacho nimekula.”

Alitaka pia kukutana na wamiliki wa maeneo ambayo yanadaiwa kuwa vituo vya biashara za dawa za kulevya akisema amepata taarifa kwamba baadhi ya maeneo yanatumika kwa biashara hiyo haramu.

Alipoulizwa kuhusu suala hilo, Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Kamishna Simon Sirro alisema mkuu wa mkoa ni mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na usalama wa mkoa, hivyo kuingilia kati suala la dawa za kulevya ni sehemu ya majukumu yake na kwamba siyo ajabu kwa mkuu wa mkoa kufanya kazi hiyo.

Kamishna Sirro na kusema leo atazungumzia suala hilo kwenye mkutano wake na waandishi wa habari.

Alipoulizwa juu ya wito huo, TID alikataa kusema lolote kwa maelezo kwamba hataki matatizo na mtu, na wasanii wengine hawakupatikana.