Makonda awashtua haki za binadamu

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda  

Muktasari:

Juzi wakati wa kuaga miili ya askari polisi watatu waliouawa na majambazi katika Tawi la Benki ya CRDB lililopo Mbande, Wilaya ya Temeke jijini Dar es Salaam, Makonda aliwaagiza polisi kuwagonga na kuwapiga wahalifu wanaowakamata wakiwamo majambazi. 

Dar es Salaam.  Tume ya Haki za Binadamu na Utalawa Bora (THBUB) imelaani kauli  ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda  ya kuliagiza Jeshi la Polisi kuwagonga na kuwapiga wahalifu wowote wakiwamo majambazi pindi wanapowakamata,

Juzi wakati wa kuaga miili ya askari polisi watatu waliouawa na majambazi katika Tawi la Benki ya CRDB lililopo Mbande, Wilaya ya Temeke jijini Dar es Salaam, Makonda aliwaagiza polisi kuwagonga na kuwapiga wahalifu wanaowakamata wakiwamo majambazi.

Mwenyekiti wa tume hiyo, Bahame Nyanduga, amesema wamemtumia Makonda barua ya wito inayomtaka afike makao makuu ya Tume Agosti 30 ili kujadili kile ilichokiona kuwa ni kejeli kwao pamoja na jumuiya yote ya watetezi wa haki za binadamu.

 “Kwa mujibu wa Kifungu cha 6(1)(f) na (i) pia Kifungu cha 27(1) na (2) (a) vya Sheria ya Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora Sura Na. 391 ya Sheria za Tanzania 2002, THBUB ina mamlaka ya kuchunguza mwenendo wa mtu au taasisi yoyote kuhusiana na utendaji wa kazi zake zinapokiuka mipaka ya madaraka yake, ili kuchukua hatua za kurekebisha ukiukwaji huo,” amesema Nyanduga kupitia taarifa iliyotumwa kwa vyombo vya habari jana.