Makontena 20 ya ‘Paul Makonda’ yana mali za Sh1.4 bilioni

Muktasari:

  • Kadhalika, barua hiyo ambayo si Mamlaka ya Mapato (TRA) wala Waziri wa Fedha na Mipan-go, Dk Philip Mpango waliothibi-tisha kuitambua, imeandikwa na mamlaka hiyo ya ukusanyaji kodi kumueleza waziri husika kuwa ombi hilo haliwezekani kwa kuwa ofisi ya mkuu wa mkoa haina sifa ya kupata msa-maha kwa mujibu wa sheria.

Dar es Salaam. Mali zilizomo ndani ya makontena 20, ambayo ni mali ya mtu anayeitwa Paul Makonda zina thamani ya Sh1.4 bilioni. Hayo yamo katika barua ili-yosambaa kwenye mitandao ya kijamii ikieleza kuwepo kwa ombi la msamaha wa kodi wa mali hizo, maombi ambayo hayastahili kuridhiwa, kwa mujibu wa Sheria ya Kodi.

Kadhalika, barua hiyo ambayo si Mamlaka ya Mapato (TRA) wala Waziri wa Fedha na Mipan-go, Dk Philip Mpango waliothibi-tisha kuitambua, imeandikwa na mamlaka hiyo ya ukusanyaji kodi kumueleza waziri husika kuwa ombi hilo haliwezekani kwa kuwa ofisi ya mkuu wa mkoa haina sifa ya kupata msa-maha kwa mujibu wa sheria.

Barua hiyo imetaja kiwango hicho cha thamani ya mali hizo, ikirejea ombi la msamaha wa kodi lililowasilishwa na ofisi hiyo ya mkoa.

Alipoulizwa kuhusu barua hiyo, mkurugenzi wa Elimu kwa Mlipa Kodi wa TRA, Richard Kayombo alijibu kuwa hawezi kuzungumzia hilo.

Pia hata waziri Mpango hakutaka kuzungumzia barua hiyo alipopigiwa simu, badala yake alisema yupo msibani hivyo hangeweza kuzungumza.

Habari za kuwepo makontena hayo zilifichuliwa na tangazo la TRA la kuwataka wamiliki wa mali zilizokaa bandarini kwa zaidi ya siku 90 kujitokeza kuzilipia na kuondoa mizigo yao, huku ikitishia kuzipiga mnada iwapo hawatatokea ndani ya siku 30.

Tangazo hilo lililochapishwa kwenye gazeti la Serikali la Daily News, lilionyesha kuwa mtu anayeitwa Paul Makonda aliagiza makontena 20 yenye mali tofauti, lakini halikueleza kama mtu huyo ni mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam.

Tayari mkuu huyo wa mkoa ameshasema kuwa hatambui mali hizo na hakuziagiza.

Hata hivyo, mwezi Februari, RC Makonda aliwapeleka baadhi ya walimu wa jijini Dar es Salaam, waandishi wa habari na wadau wengine kwenda bandarini ambako aliwaonyesha makontena yenye vifaa vya ofisi na vya kufundishia, akisema vimetolewa na Watanzania waishio Marekani.

Hata hivyo, vifaa hivyo ambavyo baadhi ni viti, meza na mbao za kuandikia, vilionekana ndani ya makontena vikiwa vimeshaunganishwa, tofauti na hali ya kawaida ya kusafirisha bidhaa zikiwa hazijaunganishwa ili kuziweka nyingi kwenye kontena moja kwa ajili ya nafasi.

Barua hiyo ya Februari 19 inamshauri waziri Mpango kuhusu msamaha wa kodi ulioombwa.

“Baada ya kupitia maombi hayo, tunapenda kukufahamisha kuwa sheria ya forodha ya Jumuia ya Afrika Mashariki ya 2004 na sheria ya kodi ya ongezeko la thamani (VAT) ya mwaka 2014 hazijatoa msamaha wa kulipa ushuru wa forodha na VAT kwa Serikali kuu na Serikali za mitaa,” inaeleza barua hiyo.

Inaeleza kuwa kutokana na sheria hiyo, ofisi ya mkuu wa mkoa ni sehemu ya serikali za mitaa na hivyo haistahili kupata msamaha.

Katika hatua nyingine, RC Makonda jana alipokea msaada wa vifaa vyenye thamani ya Sh400 milioni kutoka kwa Shubash Patel, mmiliki wa kiwanda cha MMI kwa ajili ya ujenzi wa ofisi na vyoo vya walimu. Makonda alisema kuna makontena zaidi ya 40 yanakuja kwa ajili ya kusaidia wakazi wa Dar es Salaam.

Katika hafla hiyo, Makonda alisema kuna makontena zaidi ya 40 yanakuja kwa ajili ya kuwasaidia wananchi wa jiji la DSM.

Alisema kuna makontena 16 yameshapakiwa kutoka Marekani yanakuja nchini yakiwa na samani za ofisi za walimu, mengine 10 yenye vitabu ambavyo vitatumika kujenga maktaba ya jamii.

“Kuna chuo kikuu kimoja nchini Marekani kimetenga kiasi cha dola 700,000 kwa ajili ya ujenzi wa hiyo maktaba ya jamii,” alisema Makonda.

Alisema mbali na msaada huo, alisema kuna msaada kutoka kwa Waingereza ambao ni makontena 10 yakiwa na vifaa vya matibabu kama vitanda vya wagonjwa na makontena 10 ya maziwa ya watoto wadogo.