Makontena ya Makonda sasa kugawiwa bure

Muktasari:

  • Makontena hayo yaliyokuwa yakipigwa mnada na kampuni ya udalali ya Yono yana samani mbalimbali kama viti, meza na mbao za kuandikia na yalizuiwa kutokana na kudaiwa kodi inayokadiriwa kuwa Sh1.2 bilioni.

Dar es Salaam. Baada ya minada minne iliyofanyika kushindwa kupata mnunuzi wa makontena 20 ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) sasa inafanya taratibu za kuyatoa bandarini ili kuyagawa bure.

Makontena hayo yaliyokuwa yakipigwa mnada na kampuni ya udalali ya Yono yana samani mbalimbali kama viti, meza na mbao za kuandikia na yalizuiwa kutokana na kudaiwa kodi inayokadiriwa kuwa Sh1.2 bilioni.

Kamishana Mkuu wa TRA, Charles Kichere aliliambia Mwananchi jana kuwa yatagawiwa bure hivi karibuni.

Ingawa hakutaja watakaonufaika na mgao huo, Kichere alisema Sheria ya Kodi ya Forodha ya Afrika Mashariki inaelekeza bayana kuwa mali zinazokosa mnunuzi zinawekewa utaratibu ikiwamo ule wa kugawiwa bure. “Inapojitokeza minada yote hakuna mnunuzi aliyepatikana, kuna utaratibu ulioelekezwa kisheria wa kuziondoa mali hizo sehemu ya mnada na moja ya utaratibu huo ni kugawa bure,” alisema.

Hata hivyo, hakuwa tayari kutaja tarehe ya kuondolewa makontena hayo mbali ya kusisitiza kuwa ofisi yake imeanza kukamilisha taratibu na kuna uwezekano hatima ya makontena hayo ikajulikana wiki hii.

“Nadhani haitachukua muda mrefu tutakuwa tumejua kipi tutakifanya, bila shaka ndani ya wiki hii tutakuwa tumeamua ikiwamo suala la kugawa bure,” alisema.

Alipoulizwa sababu za makontena hayo kukosa wateja, kamishna huyo alisema, “Sijui kwa nini labda nikuulize wewe maana mnazunguka huku na kule unaweza kujua.”

Alipoambiwa huenda ni kutokana na kiwango kikubwa cha bei kilichowekwa ambacho kimelamikiwa, Kichere alijibu, “Gharama au bei zinawekwa kisheria.”

“Hizi bei hatuzipangi tu kienyeji, kuna vitu vingi vinaangaliwa kabla ya kuwekwa, mfano kuna gharama ya ardhi, kuhifadhi mzigo na mengineyo. Hizi bei zipo kwa mujibu wa sheria.”

Mara ya kwanza makontena hayo yalipigwa mnada Agosti 25, lakini yalikosa wanunuzi, watu wengi walishindwa kufikia bei iliyotakiwa, baadhi wakitaja Sh10 milioni kwa kontena badala ya Sh60 milioni inayotakiwa. Baada ya makontena hayo kutouzika, Agosti 26, Makonda alitoa onyo akiwa mkoani Kagera kuwa atakayeyanunua atalaaniwa yeye na uzao wake.

Agosti 27, Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Phillip Mpango alikwenda bandarini kuyakagua na kuwataka viongozi wenzake serikalini kutathmini kauli zao na akawaomba wanaotaka kuyanunua wasiogope.

Akizungumza na madiwani, viongozi na watumishi wa Halmshauri ya Wilaya ya Chato mkoani Geita, Agosti 30, Rais John Magufuli alipigilia msumari sakata hilo akiwataka viongozi kuwatumikia wananchi bila kujali wapo kwenye nafasi gani.

“Umesikia hili sakata la Dar es Salaam, eti mkuu wa mkoa ameleta makontena, ameambiwa alipe kodi, kwa nini asilipe kodi?” Alihoji Rais Magufuli. Alisema sheria za nchi zinasema ni mtu mmoja katika nchi mwenye dhamana ya kutolipa kodi kwa mujibu wa sheria ya fedha, sheria ya madeni, sheria ya dhamana na ya misaada.

“Sasa ukichukua makontena kule umezungumza na watu wengine labda na wafanyabiashara, unasema ni makontena yako halafu ukasema tena labda ni ya walimu, wala hata shule hazitajwi maana yake nini,” alisema Rais.

“Maana yake si unataka utumie walimu ulete haya makontena, utapeleka shule mbili au tatu ndizo zitapewa, mengine unakwenda kuyauza unapeleka kwenye shoping mall (maduka makubwa). Lakini walimu walikuambia wanahitaji makochi, sofa.”

Septemba Mosi ulifanyika mnada mwingine, lakini kwa mara nyingine makontena hayo hayakuuzika kutokana na wateja kushindwa kufikia bei iliyotajwa. Kadhalika Septemba 8 ulifanyika mnada mwingine.