Makumbusho ya nyuki kujengwa Singida

Muktasari:

  • Rais wa SYECCOS, Philemon Kiemi alisema maandalizi ya ujenzi wa makumbusho hayo yaliyoanza mwaka 2013 yatachukua takriban miaka 10.

 Chama cha Wafugaji Nyuki Singida (SYECCOS), kinatarajia kutumia Sh17 bilioni kujenga makumbusho ya dunia ya nyuki ili kuboresha soko la mazao ya nyuki.

Rais wa SYECCOS, Philemon Kiemi alisema maandalizi ya ujenzi wa makumbusho hayo yaliyoanza mwaka 2013 yatachukua takriban miaka 10.

Kiemi alisema makumbusho hayo yatasaidia kuongeza idadi ya watalii kutoka nchi mbalimbali watakaojionea mbinu za ufugaji nyuki na historia nzima.

“Tunakusudia kuhudhuria mkutano wa 45 wa kimataifa wa sekta ya nyuki nchini Uturuki, utakaofanyika Septemba mwaka huu kwa lengo la kushawishi dunia kuwekeza kwenye uanzishwaji wa makumbusho hayo,” alisema Kiemi.

Alisema mpaka sasa wameshatumia Sh1.7 bilioni kuanzisha mradi huo na kwamba watawashawishi wajumbe wa mkutano huo wa dunia na wawekezaji kuanzisha kampeni ya kutafuta fedha kupitia mitandao ya kijamii inayoweza kuwafikia watu wengi duniani.

Ofisa Nyuki kutoka Wakala wa Misitu Tanzania (TFS), Mwanahamisi Mapolu alisema: “Ni mkutano mkubwa ambao unakutanisha wadau wote wa sekta ya nyuki wakiwamo watafiti, wafugaji na wanunuzi.”