Mama Magufuli aongoza sherehe Siku ya Wanawake

Mke wa Rais, Mama Janeth Magufuli 

Muktasari:

  • Ameupongeza Mkoa wa Dar es Salaam kwa kuanzisha vikundi zaidi ya 400 vya wanawake vinavyojishughulisha na usindikaji mazao, ushonaji na uchoraji.


Dar es Salaam. Mke wa Rais, Mama Janeth Magufuli leo  Machi 8, ameongoza maelfu ya wanawake wa Mkoa wa Dar es Salaam kuadhimisha kilele cha Siku ya Wanawake Duniani, huku akiziomba asasi za kiraia  na watu binafsi kushirikiana na Serikali kuwapa akina mama mbinu mbalimbali za mafunzo, mitaji na kuwatafutia masoko ya bidhaa zao.

Mama Magufuli pia ameupongeza mkoa huo kwa kuanzisha vikundi zaidi ya 400 vya wanawake vinavyojishughulisha na usindikaji mazao, ushonaji na uchoraji.

Pia ameupongeza kwa kuwa na vikundi vya kukopeshana (Vicoba) vipatavyo 2,748 ambavyo kwa pamoja vina mtaji wa jumla ya  Sh10.4 bilioni

"Ni imani yangu kuwa kama mikoa yote na taasisi nyingine za kiserikali na kiraia zitaiga mfano wa Dar es Salaam katika kuwawezesha wanawake kiuchumi pamoja na kuwashirikisha kwenye shughuli za ujenzi wa viwanda, basi tutawawezesha wanawake kiuchumi ikiwemo kushiriki kwenye shughuli za ujenzi wa viwanda", amesema.

Mama Magufuli ameyasema hayo katika sherehe hizo zilizofanyika ukumbi wa Mlimani City.

Amesema japokuwa Serikali inajitahidi kuweka usawa wa jinsia na kuwawezesha wanawake kisiasa, kiuchumi, elimu na afya, peke yake haiwezi kuzimaliza changamoto zote, hivyo ni lazima wananchi wenyewe washiriki katika kusukuma mbele gurudumu la maendeleo.

Mama Magufuli amewapongeza viongozi wa awamu zote za nchi, ikiwa ni pamoja na akina mama shupavu wa Tanu na ASP na baadaye CCM ambao kwa namna moja ama nyingine wameshiriki katika harakati za kumkomboa mwanamke nchini.

"Kutokana na umuhimu wa siku ya leo naomba nitambue mchango wa Mama Maria Nyerere, Mama Fatma Karume, Bibi Titi Mohamed, Mama Sophia Kawawa,  Hadija Jabir,  Johari Yusuf Akida, Mwajuma Koja,  Mtumwa Fikirini na wengineo wengi.

Hatuna budi kuwapongeza  akinamama hawa kwa kupigania haki za wanawake nchini," amesema.