Mama Samia awapa darasa polisi wanawake

Dar es Salaam. Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan amewataka polisi wanawake kupambana na vitendo vya uchochezi, wizi wa mitandaoni, ujangili, ugaidi na utakatishaji wa fedha.

Alisema hayo jana wakati akifunga maadhimisho ya miaka 10 ya mtandao wa polisi wanawake yaliyofanyika kwenye viwanja vya Chuo cha Taaluma ya Polisi Kurasini.

Samia alisema ulinzi ni muhimu kwa ustawi wa nchi.

“Unakuta mtu kanyanyaswa kijinsia anapofika kituoni, polisi wanasema hiyo ni aibu mkayamalize kifamilia,” alisema Samia.

Aliwataka kufuata sheria katika matukio yote ya unyanyasaji wa kijinsia badala ya kuwaacha kwenda kuyatatua kifamilia.

Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani, Hamadi Masauni aliwapongeza polisi kwa mshikamano pamoja na ujasiri waliouonyesha.

Aliwahakikishia kuwa kila kitakachopatikana serikalini kitagawanywa kwa usawa ili wafanye kazi kwa ufanisi.