Mama anayesomesha rubani kwa kuuza mkaa apata ugeni

Muktasari:

Mjane Bahati Masebu, mkazi wa Kunduchi jijini Dar es Salaam anayesomesha bintiye Nyamizi Ismail urubani kwa kuuza mkaa amesema waandishi mbalimbali wamekuwa wakipiga simu na wengine kufika nyumbani kwake


Dar es Salaam. Siku tatu baada ya Gazeti la Mwananchi kuchapisha habari za mjane, Bahati Masebu (40), mkazi wa Kunduchi jijini Dar es Salaam anayemsomesha bintiye Nyamizi Ismail (20), taaluma ya urubani kwa kuuza mkaa imewaibua waandishi wengine wa vyombo vya habari kumtembelea.

Gazeti la Mwananchi lilichapisha habari ya mama huyo kwa mara ya kwanza mwishoni mwa wiki iliyopita  likieleza jinsi anavyomudu kulipa gharama za masomo hayo ambayo ada yake inakadiriwa kuwa Sh100 milioni.

Habari hiyo imegusa hisia za watu wengi walioisoma  ambapo waandishi wa vyombo mbalimbali wameanza kumtafuta mama huyo huku wengine wakimtafuta mwandishi wa habari hiyo wakitaka kuonana na mama huyo ili wafanye naye mahojiano zaidi.

Akizungumza na MCL Digital, mama huyo amesema tangu taarifa hiyo itoke kwenye gazeti la Mwananchi Jumapili, Novemba 4,2018, amekuwa akipigiwa simu na waandishi wa vyombo mbalimbali.

Amesema baadhi ya waandishi walimwambia kuwa asiruhusu chombo au waandishi wengine wa habari wamhoji juu ya taarifa zake kwa madai kuwa wanataka tu kuuza na kupata fedha, lakini siyo kumsaidia.

“Mimi ninachohitaji zaidi kama kuna watu wanataka kunisaidia wanisaidie wasije tu hapa kunihoji na kunipotezea muda wangu, maana ninachohitaji mwanangu asome, basi. Na kama kuna mtu atataka kunisaidia anitafute kwa namna 0674-748841,” amesema mama huyo.

Kwa mujibu wa gazeti la Mwananchi, Bahati amekuwa akimsomesha mwanaye Nyamizi kwa kuuza mkaa na wakati mwingine kuomba misaada makanisani na misikitini na kwamba, ameapa lazima mtoto huyo atimize ndoto zake za kuwa rubani katika shirika kubwa nchini au nje ya nchi.

Mama huyo anamsomesha mwanaye baada ya mumewe kufariki dunia kwa ajali ya gari alipokuwa akitoka kazini mwaka 2013.

Soma zaidi: