Mambo matano yaliyojitokeza kifo cha Masogange

Muktasari:

Masogange ameweza kuwakutanisha washindani wawili wa soko la muziki wa Bongo Fleva, nao si wengine ni Diamond na Ali Kiba.


Dar/Mbeya. Tangu kutokee msiba wa Video Queen, Agnes Gerald ’Masogange’  Aprili 20, 2018, kumekuwepo na matukio mbalimbali yaliyofanyika hadi kuzikwa kwake.

Awakutanisha Diamond na Ali Kiba

Masogange ameweza kuwakutanisha washindani wawili wa soko la muziki wa Bongo Fleva, nao si wengine ni Diamond na Ali Kiba.

Katika shughuli hiyo ya uagaji iliyofanyika jana aliyetangulia ni Ali Kiba na mara baada ya kumaliza kutoa salamu zake za rambirambi, aliingia Diamond na wapambe wake na kwenda moja kwa moja meza kuu kuwasalimia watu waliokuwa wamekaa hapo akiwemo Ali Kiba.

Kitendo hicho kilisimamisha shughuli za kutoa salamu za rambirambi kwa muda na Uwanja wa Leaders Club jijini Dar es Salaam kulipuka kwa shangwe kama vile watu hawapo msibani.

Nyumba wanayoishi Uwoya na Dogo Janja yajulikana

Tangu walipofunga ndoa mwaka jana, hakuna aliyekuwa akijua wasanii Dogo Janja na Uwoya kama wanaishi nyumba moja na wapi.

Lakini msiba wa Masogange ulifichua siri hiyo, ambapo katika mahojiano yake na Mwananchi, Dogo Janja amesema anasikitika kifo cha msanii huyo, kwani alikuwa ni jirani mwema kwao na hajui ataenda kumuomba nani tena chumvi.

Amesema katika nyumba hiyo ya ghorofa inayochukua familia tano, alikuwa akiishi yeye na mke wake Uwoya, Masogange na Dogo Aslay ambaye amehama hivi karibuni.

Uwoya kujichora tattoo kumuenzi Masogange

Wakati hali ikiwa hivyo, Dogo Janja kwa Uwoya imekuwa tofauti kwani yeye hakutaka kuzungumza lolote na wanahabari kuhusiana na msiba huo kwa madai hakuwa vizuri kisaikolojia.

Hata hivyo, Uwoya ambaye alikuwa rafiki wa karibu wa Masogange, ameweza pia kuchora tattoo katika mkono wake wa kushoto na kuandika R.I.P Agnes kama njia ya kuomboleza na kumuenzi.

Mpenzi wake kuzimia na kitambaa mkononi kwaibua gumzo

Jambo lingine lililozua gumzo ni pale aliyewahi kuwa mpenzi wake, Rammy Galiz, kuonekana kwenye picha akiwa amepoteza fahamu huku akiwa ameshikilia kitambaa mkononi.

Picha hiyo imezua gumzo mitandaoni na watu kuhoji inawezekanaje mtu kazimia lakini bado kashikilia kitambaa mkononi kama si uigizaji msibani.

Hata hivyo, MCL Digital ilimtafuta Galis ambaye ni msanii wa filamu kuweza kulizungumzia hilo, ambapo alidai hakuwa amezimia bali aliishiwa tu nguvu na ndio maana hata akawa bado ana nguvu ya kushikilia kitambaa chake. 

Mtoto wa Masogange kusomeshwa hadi chuo kikuu

Mtoto wa pekee wa Masogange, Sania (11) ambaye yupo darasa la saba, kifo cha mama yake huyo kimesababisha wadau mbalimbali kujitokeza kumsaidia ili aweze kuendelea na masomo yake bila shida.

Akizungumza katika shughuli za kuaga, mweka hazina wa kamati ya maandalizi ya mazishi ya wasani walioubeba msiba huo mwanzo mwisho, Zamaradi Mketema amesema wamemuwekea Sh2 Millioni mtoto huyo kwenye akaunti yake ili zimsaidie kwenye ada atakapoanza kidato cha kwanza mwakani.

Mbali na wasanii pia jijini Mbeya wakati wa kuupumzisha mwili wa Msogange katika nyumba yake ya milele, Mmiliki wa Shule ya Sekondari ya St. Patrick ya Jijini Dar  Es Salaam, Ndele Mwaselela, ametangaza kujitolea kumsomesha mtoto  huyo  kuanzia kidato cha kwanza hadi cha nne na chuo kikuu endapo atafaulu.

Makada wa CCM Mbeya wabeba jeneza

Baada ya mwili kuwasili Mbeya, makada wa Chama cha Mapinduzi (CCM) ndio walioupokea kutoka mikononi mwa wasanii waliotoka jijini Dar es Salaam.

Mwenyekiti wa CCC Wilaya ya Mbeya, Akim Mwalupini, ndio akatoboa siri kuwa sababu ya makada hao kufanya hivyo ni kutokana na baba yake Mzee Gerald kuwa Katibu wa Jumuiya ya Wazazi Utengule Usongwe.