Mamia wajitokeza kuwazika watoto watatu wa familia moja waliofariki ndani ya gari

Muktasari:

Wananchi wameendelea kujitokeza kushuhudia mazishi ya watoto watatu waliokutwa wamefariki ndani ya gari Temeke, Dar es Salaam nchini Tanzania


Dar es Salaam. Mamia ya waombolezaji wamejaa wakisubiri kuwasili kwa miili ya watoto watatu waliofariki ndani ya gari bovu, katika mtaa wa Njaro, kata ya Temeke jijini Dar es Salaam.

Miili ya watoto hao, Jamila Mohammed (9), Amina Kunambi (7) na Yusuph Suleiman (3) ilikutwa juzi Jumanne Oktoba 16, 2018 ikiwa kwenye gari bovu aina ya Toyota Mark 2 baada ya kutoweka kwa zaidi ya siku tatu.

Akizungumza na Mwananchi leo Alhamisi Oktoba 18, 2018 Mwenyekiti wa Mtaa wa Njaro, Amina Mlewa amesema waombolezaji wanasubiri miili hiyo iwasili ili waanze taratibu za mazishi.

"Wakati wowote miili ikifika basi tutazika, awali ilibidi ipelekwe msikitini kisha makaburini lakini sasa watakuja kwanza nyumbani. Watazikwa makaburi ya Chang'ombe, Dar es Salaam," amesema.

"Tuliwatafuta sana watoto bila mafanikio juzi saa 4.00 asubuhi ndio kuna mwananchi mmoja alihisi harufu kali na wadudu wanaanguka chini toka kwenye gari, alipochungulia akaona watoto na kuanza kupiga kelele," amesema.

Mkazi wa mtaa huo, Omary Said amesema huenda kilichosababisha kifo cha watoto hao ni kukosa hewa.

"Walikuwa wanacheza kwa hiyo walipoingia ndani ya gari wakashindwa kutoka nje na kwa sababu walikosa msaada, walikufa kwa kukosa hewa," amesema.

Kati ya watoto watatu waliofariki, Jamila na Yusuph ni watoto wa mama mmoja Rukia Seif ambaye tangu apewe taarifa za msiba amekuwa akipoteza fahamu na Amina Kunambi ni mtoto wa mama mwingine, Latifa Said.