Mamia wampokea Rayvanny JNIA

Muktasari:

Kuanzia saa saba mchana vijana kutoka maeneo mbalimbali walianza kuwasili kwa makundi katika uwanja wa ndege wa Mwalimu Nyerere kwa ajili ya kumsubiri nyota huyo aliyetarajiwa kuwasili saa nane.

Dar es Salaam. Licha ya kutokuwepo kwa kiongozi yeyote wa serikali katika kumlaki Rayvanny mamia ya wakazi wa jiji la Dar es Salaam walijitokeza kwa wingi kunogesha mapokezi hayo.

Kuanzia saa saba mchana vijana kutoka maeneo mbalimbali walianza kuwasili kwa makundi katika uwanja wa ndege wa Mwalimu Nyerere kwa ajili ya kumsubiri nyota huyo aliyetarajiwa kuwasili saa nane.

Muda ulizidi kuyoyoma bila Rayvanny kuwasili lakini mashabiki hao hawakukata tamaa waliendelea kusubiri na kuimba nyimbo za kumpongeza.

Ilipofika saa tisa na robo ‘joto’ lilizidi kupanda baada ya kuwasili kwa nyota wa Wasafi Classic Baby (WCB) wakiwa wameongozwa na Diamond.

Iliwalazimu askari na walinzi uwanjani hapo kutumia nguvu kiasi kuwapanga mashabiki hao ili kuruhusu wasafiri wengine kuendelea na shughuli zao.

Saa 9:50 kelele zililipuka uwanjani hapo baada ya Rayvanny kutokeza kwenye lango la wageni wanaowasili.

Moja kwa moja nyota huyo alielekea kwenye gari maalum la wazi lililoandaliwa kwa ajili ya kumtembeza katika mitaa mbalimbali ya jiji la Dar.