Mamilioni ya fedha yawekezwa uzalishaji wa mkaa mbadala

Muktasari:

  • Mashirika hayo ya Tanzania Environmental Action Association (Teaca) na East Africa Economic Foundation (EACF) la nchini Poland kwa pamoja yamedhamiria kupunguza ukataji wa miti kwa ajili ya kuchoma mkaa na kusababisha uharibifu wa mazingira.

Mashirika mawili yasiyo ya kiserikali yanayojihusisha na utunzaji wa mazingira yametumia zaidi ya Sh300 milioni kuzalisha mkaa utokanao na masalia ya mimea.

Mashirika hayo ya Tanzania Environmental Action Association (Teaca) na East Africa Economic Foundation (EACF) la nchini Poland kwa pamoja yamedhamiria kupunguza ukataji wa miti kwa ajili ya kuchoma mkaa na kusababisha uharibifu wa mazingira.

Makamu mwenyekiti wa Teaca, Adoncome Mcharo alisema mradi huo utasaidia kurudisha mandhari ya kijani mkoani Kilimanjaro na kunusuru Mlima Kilimanjaro.

“Kutupwa na kuchomwa hovyo kwa taka ni changamoto ambayo tuliona tuifanyie kazi. Tuliona tutumiee fursa hii kuhakikisha mazingira yanaimarishwa na kulinda mlima wetu Kilimanjaro na kurudisha uoto wa asili,” alisema Mcharo.

Katika kufanikisha hilo, shule za msingi na sekondari kutoka wilaya za mkoa huo zinashirikishwa ambapo 2016/17 shule 20 zikiwamo 15 za msingi na tano za sekondari zilitekeleza mradi huo.

Mwanzilishi wa shirika hilo, raia wa Poland, Robert Zounzyk alisema lengo la mradi huo ni kuwasaidia watu wa kipato cha chini kutunza mazingira.

Alisema kuna zaidi ya miradi 30 inayotekelezwa katika nchi za Tanzania, Kenya, Burundi na Uganda na mwitiko ni mkubwa kwa kuwa watu wengi wanafahamu umuhimu wa kutunza mazingira.