Man United yachana mkeka England

KAMA uliweka ulibeti kwa kuipa ushindi Leicester City kwenye mchezo wa kwanza wa kuchana pazia la Ligi Kuu ya England msimu huu, basi utakuwa umeuchana mkeka wako kiulaini kabisa mwanangu.

Ndio! Mashabiki wengi wakiwemo wa United wenyewe hawakuwa na uhakika kama timu yao inaweza kushinda kwenye mchezo huo kutokana na kushindwa kuvunja akaunti na kufanya usajili wa maana.

Lakini, kutofanya usajili hakujawahi kuwa tatizo kwa kocha Mreno, Jose Mourinho ambaye usiku huu (jana Ijumaa) ameiongoza timu yake kuchomoza na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Leicester City kwenye dimba la Old Trafford.

Mabao mawili ya kiungo fundi wa Kifaransa, Paul Pogba na beki Luke Shaw yalitosha kumfanya Mourinho kupata usingizi mororo na kuanza kwa ushindi na kuliweka jeshi lake kileleni mwa msimamo.

Alianza Pogba aliyeiweka United mbele kwa bao 1-0 akifunga kwa mkwaju wa penalti kwenye dakika ya tatu tu ya mchezo. 

Kiungo huyo ambaye aliomba kuuzwa kwenda Barcelona, lakini mabosi wa Man United wakaweka ngumu, alipachika mkwaju huo baada ya beki Daniel Amartey kuunawa mpira kwenye eneo la hatari na mwamuzi kuamuru ipigwe penalti.

Kuingia kwa bao hilo hakukuwafanya Leicester City kuwa wanyonge na badala yake waliliandama lango la United, lakini walishindwa kutumia nafasi kadhaa walizotengeneza kwenye kipindi cha kwanza.

Mpaka kipindi cha kwanza kinamalizika, Man United ilikuwa mbele kwa bao 1-0. Kipindi cha pili kilianza kwa kasi huku Man United ikionekana kucheza kwa tahadhari zaidi na kupoza mipira ili kupunguza kasi ya wapinzani wao, ambao walikuwa moto kusaka bao.

Dakika ya 60-80 ya mchezo, mambo yalibadilika na timu zote zikishambuliana kwa zamu na dakika ya 82 Shaw akitumia juhudi binafsi aliiweka mbele zaidi United kwa kupachika bao la pili na kumpa Mourinho uhakika wa pointi tatu muhimu.

Hata hivyo, dakika ya 92, straika matata wa Leicester City Jamie Vardy aliipatia bao la kufutia machozi timu yake na kubadili matokeo kuwa 2-1.

Hadi mwisho wa mchezo, Man United ilitoka uwanjani na ushindi wa kwanza kwenye msimu mpya wa Ligi Kuu ya England.

 

REKODI MPYA EPL

Kiungo wa Manchester United, Paul Pogba ameweka rekodi katika Ligi Kuu ya England kwa kupachika bao la kwanza la msimu mpya wa ligi hiyo.

Pia, Man United imekuwa timu ya kwanza msimu huu kupata penalti tena ya mapema (dakika tatu) kwenye mchezo dhidi ya Leicester City kwenye dimba la Old Trafford mjini Manchester.

Huku kipa wa Leicester City, Kasper Schmeichel akiwa wa kwanza kuruhusu bao kwenye mechi ya kwanza ya ufunguzi wa msimu mpya wa ligi hiyo. Kisha akaruhusu pia bao la pili.

Kiungo wa Man United, Fred na beki wa Leicester City, Daniel Amartey ndio wameweka rekodi ya kuwa wachezaji wa kwanza kupewa kadi za njano.

 

VIKOSI:

MANCHESTER UNITED : De Gea; Darmian, Bailly, Lindelof, Shaw; Fred, Pogba (c), Pereira; Mata, Sanchez na Rashford.

Subs: Grant, Smalling, Young, Fellaini, McTominay, Martial, Lukaku

 

LEICESTER : Schmeichel; Amartey, Morgan (c), Maguire, Chillwell; Ndidi, Silva; Ricardo, Maddison, Gray na Iheanacho.

Subs: Ward, Evans, Fuchs, Iborra, Albrighton, Ghezzal, Vardy.