Manaibu waziri watua mgodi mpya wa rubi

Naibu Waziri wa Madini, Dotto Biteko akizungumza na wachimbaji na wanunuzi wa madini ya Ruby katika eneo la Mundarara wilaya ya Longido mkoa wa Arusha, juzi. Picha na Mussa Juma

Muktasari:

Baada ya kufika sehemu hiyo mawaziri hao waliahidi machimbo hayo yataendelea kuwa chini ya Watanzania.

Manaibu waziri wa madini, Stanslaus Nyongo na Dotto Biteko, juzi walitembelea machimbo ya madini ya rubi eneo la Mundarara wilayani Longido ambapo maelfu ya wachimbaji wadogo wamekuwa wakichimba na kununua madini hayo.

Baada ya kufika sehemu hiyo mawaziri hao waliahidi machimbo hayo yataendelea kuwa chini ya Watanzania.

Wakizungumza na wachimbaji hao ambao walianza kufurika katika machimbo hayo hivi karibuni, manaibu waziri hao walisema Serikali inawatambua na inataka madini hayo ya vito kuchimbwa na Watanzania ili kuwanufaisha wao na Taifa.

Naibu waziri Nyongo alisema Serikali inaridhishwa na uhusiano uliopo baina ya wachimbaji na wenyeji wa Kijiji cha Mundarara tofauti na maeneo mengine nchini.

Kwa upande wake, Biteko alisisitiza kuwa hakuna mfanyabiashara wa madini atakayevumiliwa kwa kutorosha madini nje ya nchi bila kulipa kodi.

Mkuu wa Wilaya ya Longido, Daniel Chongolo alisema kuanzia mwaka jana wachimbaji zaidi ya 3,000 wamejitokeza kuchimba na kununua madini hayo, jambo ambalo halijawahi kutokea tangu madini hayo yagundulike mwaka 1948.