Manusura wa ajali waeleza tairi la gari lilivyowaokoa

Muktasari:

Wakizungumza na Mwananchi jana, Domisian Manyama na Mateso Malima walisema tairi la gari ndilo lilikuwa mkombozi kwa kuwa walilishikilia hadi walipookolewa.

Dar es Salaam. “Ni miujiza”. Ndivyo unavyoweza kusema ukisikiliza simulizi za watu wawili walionusurika katika ajali ya kivuko cha Mv Nyerere kilichozama juzi mchana katika Ziwa Victoria.

Wakizungumza na Mwananchi jana, Domisian Manyama na Mateso Malima walisema tairi la gari ndilo lilikuwa mkombozi kwa kuwa walilishikilia hadi walipookolewa.

Kivuko hicho kilichokuwa kikitokea Kisiwa cha Bugolora kuelekea Kisiwa cha Ukara wilayani Ukerewe, kilizama juzi saa 8:05 mchana huku kikidaiwa kuwa kilikuwa kimepakia zaidi ya abiria 100.

Wawili hao ambao ni wakazi wa Kijiji cha Nyamanga Misheni, walilieleza Mwananchi kuwa walikuwa wakitoka Kijiji cha Bugolora ambako kulikuwa na gulio na kwamba kivuko hicho kilijaza mizigo na abiria kupita kiasi. “Kile kivuko kilikuwa na shehena ya magunia ya mahindi mbele, sasa wakati tukiwa tumebakiza mita kama 200 au 100 watu tulianza kushuka kuelekea mbele ya kivuko,” alisema Malima.

“Kwa kuwa watu walikuwa wengi na mizigo pia, upande ambao kulikuwa na shehena ya mahindi ndipo kivuko kikabinuka kutokana na kuelemewa na uzito.”

Alisema baada ya upande huo kuegama, gari zilizokuwa mbele ya kivuko hicho zilianza kuserereka na kusababisha kubinuka na kuzama.

Malima alisema tukio hilo lilitokea ndani ya muda mfupi na ilikuwa ni ghafla na bila maandalizi kwa watu kujiokoa, jambo lililomfanya kila mtu aanze kuhangaikia uhai wake.

“Mimi na mwenzangu (Manyama) wakati tukiwa tayari tumezama ndani ya maji tulibahatika kuona tairi la gari, ikabidi tuanze kuogelea kulifuata na kwenda kulishikilia hadi pale tulipokuja kuokolewa,” alisema Malima ambaye alitumia simu ya dada yake kusimulia tukio hilo baada ya ile yake kupotelea majini.

Waziri Kamwelwe

Akizungumzia ajali hiyo jana, Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Isack Kamwelwe alisema idadi ya waliofariki dunia katika hadi jana saa 10:26 jioni walikuwa watu 126, ingawa mpaka tunakwenda mtamboni ilikuwa imefika 136.

Akizungumza wakati akihojiwa na Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC), Kamwelwe alisema hadi muda huo miili 36 ilikuwa imetambuliwa na ndugu na jamaa huku kazi ya kuitambua iliyosalia ikiendelea.

Alisema jana mchana waokoaji walikuwa wamepata miili 76 na waliporejea tena kuanzia saa 10 jioni walifanikiwa kuipata mingine na kufanya idadi ifikie 126.

Jana saa 5 asubuhi, ilielezwa kuwa miili iliyokuwa imepatikana hadi muda huo ilikuwa 42, huku juzi ilipatikana 44 na kufanya idadi yake kufikia 86.

Waziri huyo aliahidi kutoa taarifa zaidi jana jioni juu ya mwelekeo halisi kama kazi ya kuopoa miili mingine itaendelea au kuahirishwa hadi leo.

“Bado kazi ya kusaka miili zaidi inaendelea. Nitazungumza tena baadaye jioni (jana) na tutaeleza kama tunaweza kuendelea na kazi hii au itatubidi kuahirisha hadi kesho (leo),” alisema waziri huyo.

Hata hivyo jana mchana kwa mara nyingine, Kamwelwe alisema uokoaji ungesitishwa saa 12 jioni.

Uokoaji

Kuhusu uokoaji, alisema wazamiaji hawajakumbana na ugumu wowote zaidi ya kukuta mizigo ambayo walilazimika kuitoa kwanza ili waweze kutoa miili.

Kamwelwe alisema kila wakati alikuwa akiwasiliana na Rais John Magufuli ambaye alikuwa akifuatilia tukio hilo hatua kwa hatua.

Waziri Mkuu akatisha ziara

Jana Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa alikatisha ziara yake ya kikazi mkoani Dodoma na kwenda Ukerewe kuwafariji wananchi waliopatwa na maafa kutokana na ajali ya kivuko hicho. “Nimelazimika kukatisha ziara yangu na wala sitakwenda Kwa Mtoro (Dodoma) ili niende kuwafariji wenzetu waliopatwa na msiba wa kupoteza ndugu zao kutokana na ajali iliyotokea jana (juzi) usiku,” alisema Majaliwa.

Maziko

Jana mchana, Waziri Kamwelwe alisema majeneza kwa ajili ya maziko yameshaandaliwa na kwamba uwepo wa majeneza hayo unaashiria kuwa shughuli ya maziko itafanyika kadri itakavyowezekana.

“Hapa leo (jana) hatulali maana nimekuja na timu nzima, jeshi lipo hapa, polisi wapo hapa na masanduku pia,” alisema.

“Shughuli za mazishi zitafanywa kwa kufuata taratibu zote ikiwemo kuzingatia mila na desturi na kwa kuzingatia taratibu za kidini kwa vile viongozi wote wa dini wapo.”

Alipoulizwa kuhusu sababu za kuzama kwa kivuko hicho, Kamwelwe alisema hawezi kulielezea jambo hilo kwa maelezo kuwa ufafanuzi utatolewa baadaye.