Viongozi, wananchi Manyara wamlilia Bendera

Muktasari:

Wamesema kuwa alikuwa mtu mcheshi, mwema na msema kweli

Babati. Wananchi na viongozi wa Mkoa wa Manyara wamemlilia aliyekuwa mkuu wa mkoa huo, Joel Bendera maarufu kwa jina la Kocha, aliyefariki jana Jumatano jioni Hospitali ya Muhimbili jijini Dar es salaam.

Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Alexander Mnyeti akimzungumzia marehemu Bendera leo Alhamisi amesema alikuwa kiongozi mchapakazi, mwadilifu, mwalimu wa kweli, mpenda watu, mcheshi na msema kweli.

Mnyeti amesema uzalendo wake upo ndani ya damu yake na uwajibikaji wake ni asilimia 100 na kwenye Taifa ni wachache waliokuwa kama marehemu mzee Bendera.

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbulu, Hudson Kamoga amesema amejifunza mengi kwa karibu zaidi marehemu Bendera akiwa mkuu wa mkoa huo.

Kamoga amesema marehemu Bendera alikuwa kiongozi mnyenyekevu wa vitendo, mwenye mapenzi makubwa kwa nchi yake na amelea viongozi wengi vijana wa nchi hii.

"Marehemu Bendera ameondoka na rekodi yake ambayo haijavunjwa kwenye nchi hii akiwa kocha pekee aliyeipeleka Taifa Stars, timu ya soka ya Taifa ya Tanzania miaka ya 1980 kwenye michuano ya kombe la mataifa ya Afrika nchini Nigeria," amesema Kamoga.

Mwandishi wa habari wa gazeti la Majira, Marry Margwe amesema tangu mwaka 2014 hadi mwezi Oktoba mwaka huu alipofanya kazi mkoani Manyara, marehemu Bendera alikuwa anafanya kazi kwa ushirikiano mkubwa na waandishi wa habari wa mkoa huo.

Margwe amesema baada ya kuingia Manyara mwaka 2014 kushika nafasi ya Elaston Mbwilo aliyehamishiwa mkoani Simiyu, marehemu Bendera aliongoza mkoa huo kwa weledi bila kubagua itikadi ya vyama vya kisiasa.

Mkazi wa mji mdogo wa Mirerani Wilayani Simanjiro, Chama Jeremia amesema marehemu Bendera alikuwa kiongozi shupavu na mdau mkubwa wa michezo na atakumbukwa na wananchi kwenye uongozi wake.