Serikali yawaonya maofisa elimu nchini

Muktasari:

  • Kwa mujibu wa takwimu za Tamisemi kuna upungufu wa walimu wa shule za msingi 85,000 nchini wakati ziada ya walimu wa masomo ya sanaa katika shule za sekondari ni 21,000.

 Serikali imewaonya maofisa elimu nchini kutowapangia walimu wa sekondari wa masomo ya sanaa kwenda kufundisha shule za msingi kwa vigezo vya kuwaadhibu, bali wazingatie vigezo vilivyowekwa.

Kwa mujibu wa takwimu za Tamisemi, kuna upungufu wa walimu wa shule za msingi 85,000 nchini wakati ziada ya walimu wa masomo ya sanaa katika shule za sekondari ni 21,000.

Akizungumza kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) na maofisa elimu wa mikoa na wilaya za Tanzania Bara leo Machi 23, Dodoma, Naibu Waziri Tamisemi, Joseph Kakunda amesema kuwahamishia walimu hao kwenda shule za msingi kunalenga kukabiliana na upungufu huo.

“Msiwapangie walimu hao wa sekondari kwenda shule ya msingi kwa kigezo cha kutoa adhabu kwa walimu bali mzingatie vigezo. Nimekwishaagiza kuwa kigezo cha mikondo ndio kiwe kigezo sahihi cha kupanga walimu. Nitalisimamia kwa karibu sana suala hili,” amesema.

Pia, amesema kigezo cha kuwapangia walimu shule za msingi kwa kutumia idadi ya wanafunzi kinazinyima shule zenye wanafunzi wachache kuwa na walimu wa  kufundisha darasa la awali hadi darasa la saba kwa ufanisi.

“Kulingana na takwimu hizo Serikali imeona ni vema walimu hawa wa masomo ya sanaa wapelekwe kufundisha shule za msingi kwani uamuzi huo wa Serikali umezingatia suala la matumizi mazuri ya raslimali watu,” amesema.

Amesema kutokana na wingi wa walimu wa sanaa katika shule za sekondari mwalimu mmoja wa sanaa alikuwa akifundisha chini ya vipindi 10 kulinganisha na mwalimu wa sekondari ambaye alikuwa akifundisha vipindi 20.

Mwenyekiti anayemaliza muda wake wa Umoja wa Maafisa Elimu wa Mikoa na Wilaya, Mayasa Hashimu ameiomba Serikali iwasisitize wakurugenzi wa halmashauri kuendelea kutenga fedha kwa ajili ya ununuzi wa magari kwa maofisa elimu wa mikoa na wilaya.

Pia ameiomba Serikali kuweka msisitizo wa pamoja katika usimamizi wa ujenzi na ukarabati wa matundu ya vyoo, vyumba vya madarasa, maabara na hosteli shuleni.

Akijibu maombi hayo kwa niaba ya Jafo, Kakunda aliziagiza halmashauri zote 185 nchini kukamilisha miundombinu ya shule za msingi na sekondari pamoja na maabara na kuwaagiza makatibu tawala wa mikoa, wakurugenzi kutenga fedha za ununuzi wa magari kupitia bajeti zao.