Maofisa elimu wapewa pikipiki, waaswa kutozifanya bodaboda

Muktasari:

  • Maofisa elimu wa kata 17 wilaya ya Mbulu, walipewa pikipiki hizo kwa ajili ya kuwarahisishia kazi wanapotembelea shule.

Mbulu. Mkuu wa Wilaya ya Mbulu Mkoani Manyara, Chelestino Mofuga amekabidhi pikipiki 17 kwa maofisa elimu wa kata katika Halmashauri ya Mji wa Mbulu, ili kuwarahisishia usafiri wa kutekeleza majukumu yao.

Akizungumza jana Septemba 11 Mofuga  amewaasa maofisa elimu wa kata kutunza pikipiki hizo na kutozifanyia biashara ya kubeba abiria maarufu kama bodaboda.

Amewataka maofisa elimu hao kuhakikisha kuwa wanazitembelea shule wanazosimamia kila mwezi ili kuongeza ufaulu wa wanafunzi kwa asilimia 100.

Pia mkuu huyo wa wilaya aliwataka maofisa elimu hao wa kata kupata mafunzo ya udereva kwa wale wasio na leseni ambayo yatagharamiwa na halmashauri ya mji huo.

Aliipongeza serikali kuu kwa juhudi kubwa ya kuwekeza katika elimu, kwani hatua ya kuwapa usafiri watumishi wa vijijini hasa maofisa elimu hao ni mafanikio makubwa mno kwenye sekta hiyo.

"Serikali ya Rais wetu mpendwa Dk John Pombe Magufuli imekusudia kuleta mapinduzi makubwa katika sekta ya elimu sambamba na viwanda ili kukuza uchumi wa Taifa kufikia uchumi wa viwanda ifikapo mwaka 2025," amesema Mofuga.

Mkurugenzi wa mji wa Anna Mbogo aliwataka maofisa elimu hao wa kata kutunza nyenzo hizo za usafiri ambazo zitakazowawezesha wao kufika maeneo mbalimbali ya kazi zao.

"Mnatakiwa kuhakikisha kuwa pikipiki hizi zinaendelea kuwa kwenye mikono ya salama ili zidumu kwa muda mrefu kwani vyombo hivyo vya moto vinahitaji kuangaliwa kwa makini," amesema Mbogo.

Mmoja kati ya wanufaika wa pikipiki hizo Julius Hotay alitoa wito kwa wamiliki wa pikipiki hizo kutumia busara pindi watakapokuwa wanatumia vyombo hivyo vya moto.

"Pikipiki hizi zinapaswa kuwa baraka kwetu na siyo laana kwani vyombo hivyo vya moto vimewasababishia majeraha na vifo kwa watu wengi wanaovitumia bila kuchukua tahadhari kwa kukimbia ovyo pasina sababu," amesema Hotay.