Maofisa Nemc wakabiliwa na mashtaka matatu

Muktasari:

Washtakiwa wamekana mashtaka ambayo upelelezi wake unaelezwa haujakamilika.

 

Dar es Salaam. Maofisa wawili wa Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (Nemc), wamepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakikabiliwa na mashtaka matatu likiwemo la kughushi.

Wakili wa Serikali, Narindwa Sekimanga mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi amedai leo Alhamisi Desemba 7,2017 kuwa washtakiwa ni Andrew Kalua na Arnold Kisiraga ambao wanadaiwa kula njama ya kutenda kosa, kughushi na kuwasilisha nyaraka ya kughushi.

Washtakiwa wanadaiwa kati ya Machi Mosi,2017 na Julai 31, 2017 katika maeneo ya Mikocheni wilayani Kinondoni, Dar es Salaam, walikula njama na mtu mwingine ili kufanya kosa la kughushi.

Wanadaiwa kati ya Machi Mosi,2017 na Julai 7,2017 eneo la Mikocheni kwa nia ya kudanganya walighushi nyaraka.

Inadaiwa walighushi muhtasari wa kamati ya ushauri ya sekta iliyopitia kikao cha kampuni ya East Coast Liquid Storage Limited iliyoko kiwanja namba 231 Kurasini wilayani Temeke, Dar es Salaam ya Juni 16,2017 kuonyesha kamati ya ushauri wa kitaalamu iliyokaa Aprili 11,2017 katika ukumbi wa Nemc na kuazimia wazungumzie upungufu ulioonekana huku wakijua si kweli.

Kalua anadaiwa Juni 16,2017, aliwasilisha nyaraka ya kughushi kwa Cecilia Toto Douglas. Washtakiwa walikana mashtaka ambayo upelelezi wake unaelezwa haujakamilika.

Hakimu Shaidi alitoa masharti ya dhamana kwa kila mshtakiwa kuwa na wadhamini wawili wenye barua za utambulisho ambao kila mmoja atasaini bondi ya Sh5 milioni.

Washtakiwa walikamilisha masharti na kuachiwa huru kwa dhamana. Kesi imeahirishwa hadi Januari 11,2018.