Maombi yafanyika katikati ya barabara kuepusha ajali

Wazee wa kimila na machifu wa kabila la Wasafwa wakitembea katika barabara kuu ya Tanzania – Zambia walipokuwa wakishuka Mlima Igawilo jijini Mbeya jana. Wazee hao walikuwa wakifanya tambiko la kuzuia matukio ya ajali katika eneo hilo. Picha na Ipyana Samson

Muktasari:

  • Hivi karibuni, mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Amos Makalla aliwataka viongozi wa dini na kimila kushiriki katika maombi ili Mungu auepushe mkoa huo na ajali.

Mbeya. Mfululizo wa matukio ya ajali mkoani hapa umewakutanisha waumini wa Kanisa la The Pool of Siloam waliofanya maombi kuombea barabara ili ajali zikome.

Hivi karibuni, mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Amos Makalla aliwataka viongozi wa dini na kimila kushiriki katika maombi ili Mungu auepushe mkoa huo na ajali.

Zaidi ya watu 40 wamefariki dunia katika kipindi cha wiki tatu kutokana na ajali za barabarani kati ya Juni 14 na Julai 5.

Kutokana na ajali hizo, waumini wa The Pool of Siloam wakiongozwa na kuhani msimamizi wa Njia ya Magharibi ya kanisa hilo, Wisdom Shangwe walikusanyika jana asubuhi katika eneo la mteremko wa Mlima Iwambi-Mbalizi kwenye barabara kuu ya Tanzania-Zambia ilikotokea ajali Julai Mosi na kusababisha vifo vya watu 20 na majeruhi 45.

Waumini hao walisimama katikati ya barabara hiyo kwa muda wa dakika 15 kufanya maombi maalumu huku wakiwa wameshika maji kwenye chupa na baadaye waliyamwaga barabarani.

Kwa mujibu wa waumini hao maji hayo wanaamini kwamba ni damu ya Yesu itakayotumika kuzuia pepo linalosababisha ajali mkoani hapa.

Akizungumza baada ya kufanya maombi, Kuhani Shangwe alisema waliamua kwenda eneo la mteremko wa mlima huo kufanya maombi kwa lengo la kuwakilisha maeneo yote ambayo ajali hutokea mara kwa mara.

Aliyataja maeneo hayo kuwa ni mteremko wa mlima Igawilo katika barabara kuu ya Tanzania-Malawi, Kawetele (barabara ya Mbeya mjini-Chunya) na mteremko wa Mlima Nyoka-Uyole jijini Mbeya.

“Yale siyo maji tuliyoyamwaga mahala hapa kama unavyodhani, neno la Mungu linasema kwamba tunao uwezo wa kubadili maji kuwa damu,” alisema Shangwe.

“Hivyo kwa imani tuliyo nayo sisi, maji yale unaweza kuyabadilisha yakawa damu ila hutayaona kwa macho kwa sababu ukisoma neno la Mungu unaambiwa vinywa vyetu vinatoa moto.”

Wakati waumini hao wakiwa mlima Iwambi-Mbalizi, machifu na wazee wa kimila zaidi ya 20 walionekana wakifanya tambiko katika barabara ya Mbeya-Kyela eneo la mlima Igawilo katika sehemu ambayo ilipoteza maisha ya watu watano na wengine kadhaa kujeruhiwa.

Mwananchi liliwashuhudia machifu hao wakiwa wamevalia mashuka meusi wakiongozwa na chifu mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Roketi Mwashinga wakizunguka eneo la mteremko wa mlima huo huku wakiimba nyimbo za asili za kabila la Wasafwa kila baada ya kutembea hatua 10.

Wakati machifu na wazee hao wa kimila walikuwa wakiimba, machifu wawili wanawake walipiga vigelegele.

Pia katika tukio hilo machifu wawili walionekana wakiwa wameshika kuku mmoja mmoja na panga mkononi.

Hata hivyo, viongozi hao wa kimila hawakuwa tayari kuzungumza chochote na wanahabari.

Ombi la Makalla

Wiki iliyopita, mkuu wa mkoa, Makalla alikutana na viongozi wa dini zote ofisini kwake na kukubaliana jana kufanya maombi ya pamoja katika Viwanja vya Ruanda Nzovwe.

Ombi hilo la Makalla lilifuatia ajali ya Julai 5, iliyoua watu watano ikihusisha lori kulalia magari madogo.

Pia, Julai 2 lori liliangukia mabasi madogo matatu na kusababisha vifo vya watu 20.

Juni 14, watu 13 walifariki dunia wakiwamo vijana 11 waliokuwa mafunzoni katika Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), ajali iliyotokea kwenye mteremko wa Igodima.