VIDEO: Maombi yatua, Maua Sama, wenzake wafikishwa mahakamani

Muktasari:

Msanii Maua Sama na wenzake walishikiliwa na polisi kwa takribani siku tano, wakili wao Ijumaa Septemba 21, 2018 aliwasilisha ombi mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu akitaka wateja wake wapewe dhamana kwa kuwa mashtaka yanayowakabili yanadhaminika

Dar es Salaam. Maombi yaliyowasilishwa na wakili Jebra Kambole anayewatetea msanii Maua Sama na wenzake katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu yatasikilizwa Septemba 26, 2018.

Kambole aliwasilisha maombi hayo dhidi ya Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP), Mkuu wa Jeshi la Polisi, Inspekta Jenerali Simon Sirro na mkurugenzi wa makosa ya Jinai Kanda Maalum (ZCO).

Katika maombi hayo yaliyowasilishwa Septemba 21, 2018, Kambole ameomba watu saba wanaoshikiliwa na Jeshi la Polisi  kwa zaidi ya wiki moja, kupelekwa mahakamani  na kusomewa mashtaka yanayowakabili sambamba na kupewa dhamana.

Maombi hayo yalifikishwa leo Septemba 24, 2018 mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Huduma Shaidi ambapo wakili Kambole   aliomba watu hao saba wafikishwe mahakamani ili wasomewe mashtaka yanayowakabili na wapatiwe dhamana.

Hata hivyo, wakati hayo yakiendelea watu hao walikuwa hawajafikishwa mahakamani.

Mbali na Mausa Sama, wengine ni watangazaji Shafii Dauda na Sudi Kadio maarufu Soudy Brown, Michael Mlingwa, Fadhili Kondo (meneja wa Maua), mshehereshaji Antony Luvanda na Benedict  Kadege.

Upande wa mashtaka uliwakilishwa na wakili wa serikali,  Tumain Kweka ambaye  aliomba kupewa siku tatu ili waweze kuwasilisha majibu ya hati kinzani kwa maandishi.

Pia aliongeza kuwa waleta maombi waliyaleta maombi hayo na kuwapatia.

Baada ya kusikiliza hoja hizo, Hakimu Shaidi  aliamuru upande wa mashtaka kuwasilisha majibu kinzani kwa maandishi Septemba 25 na kwamba maombi hayo yatasikilizwa rasmi Septemba 26 na kuagiza siku hiyo washtakiwa waletwe mahakamani.

Hata hivyo,  muda mfupi baadaye waleta maombi hao waliletwa mahakamani hapo na kuhifadhiwa mahabusu.