Mapambano kuokoa mto Ruaha Mkuu yaanza Mbeya

Muktasari:

  • Agizo hilo limetolewa na kikosi kazi cha kitaifa cha kunusuru ikolojia ya mto Ruaha kilichoko mkoa wa Mbeya.

Mbeya. Kampuni ya Highland Estates inayolima mpunga wilayani Mbarali imepewa agizo la kusafisha mifereji yote inayozunguka shamba lao ili kuruhusu maji kupita kwa urahisi kwenda mto Ruaha.

Agizo hilo limetolewa na kikosi kazi cha kitaifa cha kunusuru ikolojia ya mto Ruaha kilichoko mkoa wa Mbeya.

Pia wametakiwa kuanza taratibu za kupatiwa cheti cha ukaguzi wa athari za mazingira kitoka Baraza la Taifa la Usimamizi wa Mazingira (NEMC).

Mwenyekiti wa kikosi kazi hicho, Richard Muyungi alisema uongozi wa shamba hilo wafanye juhudi za ziada kutunza mazingira yote yanayozunguka shamba hilo na kuhakikisha maji yanapita kwa urahisi katika mifereji ya matoleo ya kupeleka maji mto Ruaha Mkuu.

"Tunawapa mwezi mmoja  mfanye ukarabati na mrekebishe hali ya usafi katika mifereji  ya shamba lenu baada ya muda huo tutarudi kwa ajili ya kukagua." amesema Muyungi

Kikosi kazi hiko pia kilitembelea katika shamba la Kapunga Rice Project na kujionea matumizi mabaya ya maji kwa  kuyachepusha bila vibali  kunakofanywa na wananchi walio maeneo ya jirani.