Mapato ya jiji la Arusha yafikia Sh 13.8 bilioni

Mkurugenzi wa Jiji la Arusha, Athuman Kihamia

Muktasari:

Ongezeko hilo linatokana na usimamizi mzuri wa fedha za jiji na matumizi ya mashine za kukusanya mapato za kielekroniki

Arusha. Mapato ya Halmashauri ya Jiji la Arusha, katika kipindi cha miaka miwili  yameongezeka kutoka Sh 10 bilioni mwaka 2014/15 hadi kufikia Sh 13.8 bilioni mwaka 2016/17 kutokana sababu kadhaa, ikiwepo kuboresha mfumo wa  makusanyo  ya mapato kwa kutumia mashine za kielekroniki.

Akizungumza na Mwananchi leo Alhamisi, Mkurugenzi wa Jiji la Arusha, Athuman Kihamia amesema ongezeko hilo linatokana na usimamizi mzuri wa fedha za jiji na matumizi ya mashine za kukusanya mapato za kielekroniki.

Alisema jiji lilikuwa limepanga kukusanya kiasi cha Sh 12.3 bilioni katika mapato ya ndani na nje lakini sasa wamefanikiwa kuzidi malengo ambayo walijipangia.

 

Kihamia alisema ongezeko la mapato hayo  limetokana pia na kudhibiti udanganyifu, kuwepo usalama wa fedha na utunzwaji mzuri wa kumbukumbu za walipa kodi.

"Ukusanyaji wa mapato haya umewezesha jiji kutumia asilimia 60 ya mapato yake ya ndani katika miradi mbalimbali ya maendeleo, kutoa mikopo kwa akina mama na vijana na asilimia 40 kutumia katika huduma za wananchi," amesema.

Amesema hadi kufikia Juni, 2017 mikopo yenye thamani ya Sh1.3 bilioni imetolewa kwa vikundi vya akina mama na vijana na miradi kadhaa imetekelezwa ikiwepo ukarabati wa dambo la Murieti na ununuzi wa magari maalum ya taka.

"Tuna malengo kadhaa kama jiji na miongoni mwa hayo ni Arusha kuwa mji mkuu wa kijani na utalii katika ukanda ya Afrika Mashariki na dhima ya kuwa na jamii yenye uchumi mpana, mawasiliano ya uhakika na usafi wa mazingira," amesema